Meya wa manispaa ya Kigoma Ujiji Baraka Lupoli akizungumza kwenye kikao hicho cha baraza (kulia aliyekaa) Mkurugenzi wa manispaa ya Kigoma Ujiji Mwantumu Mgonja
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
MADIWANI katika halmashauri ya manispaa ya Kigoma Ujiji wameutaka uongozi wa manispaa hiyo na jeshi la polisi kuchukua hatua Madhubuti kukabiliana na wimbi la wasichana wanaojiuza (Machangudoa) ambao wanaharibu taswira nzuri ya heshima na Adamu ya wakazi wa mji huo.
Wito huo wa madiwani umetolewa kwenye kikao cha kawaida cha baraza la madiwani la Halmashauri ya manispaa ya Kigoma Ujiji wakati madiwani hao wakijadili taarifa ya kamati ya kudhibiti ukimwi ambayo imegusia kuwepo kwa wimbi kubwa la wasichana hao.
Akizungumzia hali hiyo diwani wa kata ya Mwanga Kusini, Mussa Maulid alisema kuwa kila inapofika jioni wasichana hao wanajipanga barabarani kwa ajiili ya kutafuta wateja kwenye baadhi ya nyumba za kulala wageni ambazo zinafahamika kwa wasichana hao kuuza miili yao.
Maulidi alisema kuwa wasichana hao kwa sasa wamechukua vyumba kwenye baadhi ya nyumba hizo za kulala wageni (zinafahamika) wakifanya ndiyo makazi yao na wateja ambao wanataka kumaliza shughuli zao kwenye vyumba vya wasichana hao hupangiwa kiwango cha kutoa bila uficho.
Naye Diwani wa kata ya Buhanda, Kilahumba Lutuli alisema kuwa kuwepo kwa wimbi kubwa la wasichana wanaouza miili yao kwenye manispaa hiyo wakifanya shughuli zao bila kificho ni hatari kwa afya za watu hivyo akataka hatua zichukuliwe kuokoa jamii na hatari hiyo.
Hata hivyo kwa upande wake diwani wa kata ya Rubuga,Omari Gindi akizungumzia wimbo hilo la madada poa ametaka wasichana hao kuwekewa mazingira ambayo yatawafanya kufanya shughuli zao bila kuhatarisha afya za watu badala ya kuwafukuza au kuwaondoa kwani wamekuwa wafariji wakubwa wa watu wenye matatizo na familia zao.
Akihitimisha mjadala huo Meya wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Baraka Lupoli alisema kuwa wasichana hao ni tatizo hivyo idara ya afya na polisi lazima watafuta namna ambayo itawafanya wanakabiliana na wimbi hilo hasa kutoka nchini Burundi ambao wanaishi kwenye nyumba za kulala wageni kwa muda mrefu na kufanya makazi yao.
0 Comments