Na Hamida Ramadhan,Matukio Daima App Dodoma
SHEIKH wa Mkoa wa Dodoma, Alhaj Dkt. Mustapha Rajabu Shaaban, amewataka Watanzania kuendelea kuilinda na kuienzi amani ya taifa, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Desemba mwaka huu.
Akizungumza katika Swala ya Eid El Hajj iliyofanyika jijini Dodoma, Sheikh Dkt. Rajabu alisema kuwa ndani ya masiku kumi matukufu ya ibada hiyo, waumini na Watanzania kwa ujumla wanapaswa kutumia muda huo kuiombea nchi iendelee kuwa na utulivu na mshikamano.
“Amani yetu ni jambo la msingi sana. Katika Qur’an, suala la amani limetangulizwa mbele hata ya riziki. Bila ya amani, hatuwezi kufanya biashara, kusoma, wala kutekeleza ibada zetu. Hii ni tunu ya taifa, tunapaswa kuilinda kwa nguvu zote,” alisema Sheikh Rajabu.
Sheikh huyo alitoa mfano wa mataifa mengine yaliyoathirika kutokana na kukosekana kwa amani kama vile Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Gaza, ambako alisema wananchi wake huishi kwa hofu hata wakati wa kufanya ibada.
“Wenzetu wakiswali wanafanya hivyo kwa wasiwasi mkubwa kwa sababu ya vurugu na migogoro. Ni wajibu wetu kama Watanzania kuhakikisha hali kama hizo hazitokei nchini mwetu,” aliongeza.
Aidha, Sheikh Dkt. Rajabu alionya kuhusu baadhi ya watu wanaochochea vurugu kwa maslahi yao binafsi huku wakiwa na uwezo wa kukimbilia nje ya nchi, na kuwaacha wananchi wa kawaida wakibeba gharama za migogoro.
“Wapo watu wanaotaka kuivuruga nchi lakini wao wana uwezo wa kukimbilia nje. Hawa wasipewe nafasi, wala kusikilizwa. Tusimame kwa pamoja kuitetea amani yetu,” alisisitiza.
Sheikh Rajabu alihitimisha kwa kuwasihi Watanzania wa dini zote kushirikiana kuiombea nchi na kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani, haki na utulivu, kwa maslahi ya sasa na vizazi vijavyo.
0 Comments