Header Ads Widget

BOSI IPTL ATAKA SULUHU NA SERIKALI KUNUSURU UZALISHAJI UMEME

 


Mkurugenzi na Mjumbe wa Bodi ya IPTL, James Yarah kushoto, akiwa na aliyekuwa mfanyakazi wa Kampuni hiyo, Clement Beatus wakionyesha moja ya mashine ya kudhibiti mafuta ya kuendesha mtambo iliyofunguliwa na kuibwa vifaa mbalimbali.

NA MATUKIO DAIMA APP, DAR

MKURUGENZI na Mjumbe wa Bodi ya Kampuni ya Kuzalisha Umeme wa Dharura (IPTL), James Yarah amesema wako tayari kukaa chini na Serikali ili kukinusuru kiwanda kwani kiko katika hali mbaya, kianze kufanyakazi  kwa maendeleo ya Taifa.


Yarah akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya menejimenti ya IPTL jana Februari 13, 2024 kiwandani hapo alisema ili kunusuru mtambo huo kiasi cha Dola za Marekani milioni 30 zinahitajika kufanya ukarabati na kuanza awamu ya kwanza ya uzalishaji wa Mega Wati 50.


"Tunamuomba Rais Samia Suluhu Hassan akubali maombi yetu ya kukaa mezani kama ilivyofanyika kwa Symbion,"alisema Yarah .


Mtambo ya IPTL wenye vinu 10 vyenye uwezo wa  kuzalisha umeme wa Mega Wati 100 ulisimama kwa agizo la Serikali Juni 2017 na kusababisha kuwa katika hali chakavu.


 “Dola Milioni 30 tunazoziomba ni sawa na Sh  7,620,000,000 bilioni, tunamuomba Rais aiangalie IPTL kwa jicho la huruma. Tuko tayari kukaa meza moja na Serikali.


"Hali ya  mtambo wetu kwa sasa ni mbaya, umechakaa, vifaa mbalimbali vinaibwa na eneo lake kugeuka pori, jambo linalosababisha thamani ya uwekezaji kuendelea kushuka siku hadi siku,”alisema.


Mkurugenzi Yarah alisema hadi mtambo huo unafungwa Juni,  2017  thamani ya kiwanda  ilikuwa  Sh 250, 237,000,000, kutokana na uharibifu uliojitokeza kwenye kila eneo la uwekezaji ni wazi kwamba thamani hiyo imeshuka.


Alisema Serikali ikiwapatia kiasi cha fedha wanazoomba wana uwezo wa kurudisha kiwanda hicho katika hali yake ya awali ndani ya miezi mitatu na kuzalisha  awamu ya kwanza Mega Wati 50 kwa miezi sita ya awamu ya kwanza  kwa kuwasha vinu (injini) tano  jambo ambalo litasaidia kukoma kwa tatizo la mgao wa umeme  nchini.


Alisema kabla ya mtambo huo kusitishwa, kiasi cha Megawati 100 zilikuwa zinazalishwa na injini 10 za kiwanda hicho na kuingizwa kwenye gridi ya taifa ili kuimarisha nishati ya umeme katika Mkoa wa Dar es Salaam, Arusha na  Zanzibar.


“Rais wetu anapambana kila kona duniani kuimarisha mahusiano kwa nia ya kuongeza wawekezaji, juhudi zake zitaendelea kuzaa matunda ikiwa taifa litakuwa na umeme wa uhakika,"alisema.


IPTL ilikoma uzalishaji mwaka 2017 baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati  na Maji (EWURA) kusitisha leseni ya uzalishaji. Tangu wakati huo kiwanda hicho kipo chini ya Serikali.


Mwisho

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI