Header Ads Widget

MAANDALIZI YA TAMASHA LA CIGIGO MUSIC FESTIVAL 2025 YACHUKUA SURA MPYA


 Na. Andrew Chale Matukio Daima App.

Chamwino, Dodoma – Taasisi ya Chamwino Arts Centre imeanza kwa kasi maandalizi ya "Cigogo Music Festival 2025", tamasha maarufu linalolenga kudumisha, kuendeleza na kutangaza urithi wa kitamaduni wa jamii ya Wagogo kupitia muziki, ngoma na sanaa za asili.

Katika hatua za awali za maandalizi, timu ya uongozi kutoka Chamwino Arts Centre(CAC) imekuwa ikifanya ziara za kimkakati kutembelea vikundi mbalimbali vya ngoma vya asili vilivyopo katika maeneo tofauti ya Wilaya ya Chamwino na Mkoa mzima wa Dodoma. Lengo kuu la ziara hizi ni kufuatilia utayari wa vikundi hivyo, kuwahamasisha washiriki wapya, na kupanga kwa kina shughuli zitakazojumuishwa kwenye tamasha hilo la kipekee.

Tamasha la mwaka huu, linalotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 25 hadi 27 mwezi Julai 2025, linatarajiwa kuwavuta wasanii wa ngoma, watunzi wa nyimbo za asili, vikundi vya utamaduni na wadau wa sanaa kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania na hata nje ya nchi, zaidi ya vikundi HAMSINI(50) vyenye kuleta jumla ya wasanii elfu moja(1000) vinatarajiwa kushiriki. 



Kupitia tamasha hilo, Chamwino Arts Centre (CAC) inalenga kuonesha utajiri wa urithi wa jamii ya Wagogo, kukuza vipaji vya vijana, na kuchochea utalii wa kiutamaduni kama nyenzo ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Mwaka huu maandalizi yamezingatia ubunifu zaidi, ushirikishwaji wa jamii kwa kiwango kikubwa, na matumizi ya teknolojia katika kuhifadhi, kurekodi na kutangaza maudhui ya tamaduni za asili.

“Tamasha hili ni zaidi ya burudani – ni jukwaa la heshima kwa tamaduni zetu, daraja la vizazi na darasa la historia ya Wagogo. Tunaamini mwaka huu litakuwa la kipekee zaidi,” amesema Mkurugenzi wa kituo hicho, Bw.Naamala Samson.

Cigogo Music Festival limeendelea kuwa moja ya matukio muhimu ya kalenda ya kiutamaduni nchini, likiwa linachangia katika kulinda urithi wa kitaifa na kuhimiza mshikamano kupitia sanaa.








Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI