Na Gabriel Kilamlya Matukio DaimaAPP NJOMBE
Jeshi la polisi mkoani Njombe limekiri kuwa Wilaya ya Ludewa ingali inaongoza kwa mauaji yanayochagizwa na Imani za kishirikina ukilinganisha na wilaya nyingine.
Mbele ya vyombo vya habari wakati akitoa ripoti ya utendaji kazi wa jeshi la polisi katika kipindi cha mwezi Disemba hadi sasa Kamanda wa Polisi mkoa wa Njombe Mahamoud Banga amesema Katika utafiti alioufanya kupitia taarifa za jeshi hilo kwa kipindi cha miaka mitatu amebaini mauaji mengi katika wilaya ya Ludewa yanahusishwa na Imani za kishirikina tofauti na wilaya nyingine jambo ambalo hatua za makusudi zinapaswa kuchukuliwa kwa kila kada.
Kutokana na hatua hiyo kituo hiki kimezungumza na Wise Mgina mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Ludewa pamoja na Edgar Mtitu Diwani wa Kata ya Lubonde wilayani humo ambao wanasema pamoja na kuwapo kwa vitendo hivyo lakini kila mmoja anapaswa kuwajibika katika kutoa haki kwa wananchi.
Baadhi ya wananchi mkoani Njombe wanasema bado uelewa ni mdogo katika jamii na ndio sababu imeendelea kuwaamini wapiga ramli chonganishi huku wakitaka vyombo vya dola kuwachukulia hatua kali za kisheria waganga wachonganishi.
Mauaji hayo yamekuwa mwiba katika ukuzaji maendeleo katika taifa kwani baadhi ya wananchi watashindwa kufanya maendeleo wakihofia Kurogwa.
0 Comments