Header Ads Widget

WATOA HUDUMA ZA AFYA ZINGATIENI MAADILI

Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima App Dodoma.

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya imewataka watoa huduma wote wa Afya kuhakikisha wanazingatia  suala zima la ubora wa huduma na maadili ili wananchi wafurahie huduma wanazozipata. 


Kauli hiyo imetolewa leo jijini hapa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt, Grace Maghembe wakati wa mkutano wa kuboresha huduma kwa wateja na mawasiliano bora kuanzia ngazi ya awali kwa mteja uliowahusisha madaktari na wauguzi Tanzania bara na Zanzibar

Dkt, Maghembe amesema Sekta ya Afya ni sekta nyeti na imekuwa ikigusa maisha ya mwananchi moja kwa moja kuanzia mtaa, kijijini hadi juu hivyo ubora wa huduma ni muhimu kwa wahudumiwa. 


Kwenye suala zima la utoaji wa elimu kwa watoa huduma wameshafika Mikoa nane ambapo lengo ni kufikia Mikoa 12 na Halmashauri zake  na baadae nchi nzima.

"Kikubwa tuonyeshe utofauti kwa kufuata nidhamu,heshima na viapo vyetu vya maadili kwani serikali imefanya maboresho makubwa kwenye miundombinu, kuajiri wataalamu na suala zima la kununua vifaa na vifaa tiba vya kisasa na mafunzo kwa watumishi bila kusahau huduma za dharura na uangalizi maalumu ICU huduma za msingi karibu kwenye hospitali zote hapa nchini, " Amesema Dkt,Maghembe. 


Na kuongeza " Kikao chetu leo kinalenga kuhakikisha ubora wa huduma ambapo wauguzi na madaktari sasa wanakwenda kufanya huduma Bora kuanzia getini anapoingia mgonjwa hadi anapotoka amepokelewaje amepewa huduma, " Amesema . 

Amewahakikishia wananchi  kuanzia sasa pamoja na maboresho yote yaliyofanyika watajikita katika ubora wa huduma ili maboresho ya vifaa miundombinu watumishi yaendane na ubora wa huduma na wananchi wafurahie huduma na kupewa huduma kulingana na matatizo yao kulingana na makundi yao mbalimbali. 


Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi anayesimamia Ubora wa Huduma za Uuguzi na Ukunga kutoka Wizara ya Afya Saturini Manangwa aliwataka watoa huduma nchi nzima kuanza kujiandaa na kujielekeza katika kutoa huduma zenye utu, maadili na heshima.


Amesema kuwa wanaanza na mikoa nane ya mfano na watazifikia Halmashauri zote nchini pamoja na vituo vyote vya kutolea huduma ikiwa ni awamu ya kwanza ya mwaka wa fedha.


Alifafanua kuwa hiyo itakuwa kama mfano ya kuona namna ya kwenda kuendeleza katika mikoa mingine iliyobaki.


" Sisi kama Wizara ya Afya tunachukua fursa hii kuwashukuru wadau wa maendeleo hasa Shirika la UNICEF kwa kuungana na serikali katika kuinarisha utoaji wa huduma  pamoja na kuboresha huduma kwa kuangalia eneo la kuhudumia mteja kwa kuzingatia utu, maadili na heshima na upendo," amesema.


Ameongeza kuwa hicho ni kikao cha awali na kwamba wanajipanga kwa pamoja kuhakikisha wanaenda kujenga uwezo wa mifumo ya kutoa huduma  kwa watoa huduma wa afya kuhakikisha kila mteja anayefika anapokelewa kwa ukarimu.


Ameeleza kuwa wanafanya maboresho makubwa katika sekta hiyo na watajenga uwezo kuhakikisha mteja anapofika anapokelewa kwa ukarimu na kuelekezwa namna ya kupata huduma na kujikita zaidi kwenye kuboresha mawasiliano ya watoa huduma na wateja.


Mkurugenzi huyo amesema pia watashughulikia changamoto ndogo ndogo ikiwamo kuchelewa kupata huduma na kwamba watajikita kwenye changamoto hizo na watajenga uwezo kwenye ngazi zote na kujielekeza katika huduma za msingi kuanzia ngazi ya Halmashuri kushuka chini.


Mtaalumu wa Ubora wa Huduma kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia watoto na wanawake katika mataifa yanayoendelea(UNICEF) Shally Mwashemele amesema kuwa Shirika hilo linashirikiana na serikali kwa upande wa huduma ya mama na watoto kuanzia wachanga.

"Tupo hapa kuhakikisha wateja wanapata huduma zenye utu, maadili na heshima pia UNICEF inaisaidia serikali kuhakikisha mtu yoyote anapata huduma na sio mama na mtoto tu,"alieleza Mwashemele.


Naye Msajili wa Baraza madaktari Tanzania (MCT),David Paul alisema ni jambo ambalo kwa sehemu kubwa walikuwa wakilifanyia kazi bila kuwa na msisitizo ambapo kwa sasa kama wizara wanataka kuweka msisitizo huo wa ubora wa huduma


Amesema kuwa utoaji wa huduma za afya una mitazamo ya aina mbili  ya watoa huduma wenye kwa maana ya Sayansi na elimu waliyoipata na taaluma yao ambayo inawahitaji kufanya kutokana na miongozo pamoja na viwango walivyowekwa.


Msajili huyo ameongeza kuwa sehemu ya pili ni mtazamo wa mwananchi au mteja wanaye hudumiwa ambapo ndio sehemu hiyo ya huduma yenye heshima kwenda kufanya kwa sehemu kubwa.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI