Katibu wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa Oganaizesheni, Issa Gavu akizungumza kwenye mkutano mkuu wa jimbo la Muhambwe wilaya ya Kibondo mkoa Kigoma.
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
MBUNGE wa jimbo la Muhambwe wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma Dk.Florence Samizi amejivunia kazi kubwa aliyofanya ya kuleta maendeleo kwa wananchi kwenye jimbo hilo ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi wa CCM.
Dk.Samizi alisema hayo Akitoa taarifa ya utekelezaji wa kazi mbalimbali alizofanya kwenye jimbo hilo tangu achaguliwe kuwa mbunge mwaka 2020 kwenye mkutano Mkuu wa jimbo hilo ambao pia ulihudhuriwa na Katibu wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa Oganaizesheni, Issa Gavu na Mkuu wa mkoa Kigoma,Thobias Andengenye.
Mbunge huyo wa jimbo la Muhambwe alisema kuwa amefanya kazi kwa kuchochea maendeleo ya jimbo kwa kutoa fedha kutoka vyanzo mbalimbali ikwemo kiasi cha shilingi milioni 152 kutoka mfuko wa jimbo ambapo Pamoja na kuhamasisha wananchi kushiriki shughuli za maendeleo yeye binafsi pia ameshiriki kwenye shughuli mbalimbali za jimbo hilo.
Samizi alisema kuwa kazi aliyofanya kwa kipindi hicho imewezesha utekelezaji wa miradi mikubwa katika sekta ya elimu ikiwemo ujenzi wa shule mpya za msingi na sekondari, ujenzi wa madarasa,vyoo,mabweni,ofisi za walimu na nyumba za walimu huku miradi ya maji ikiwa sehemu ya kipaumbele ya utekelezaji wa miradi yake.
Sambamba na hilo alisema kuwa kazi kubwa pia imefanyika kwenye sekta ya afya kwa kuimarisha miundo mbinu ya huduma kwenye vituo vya huduma vilivyokuwepo, ujenzi wa zahanati mpya vijijini na kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miundo mbinu ya barabara vijijini na suala la kupeleka umeme kwa wananchi vijijini.
Aidha mbunge huyo alisema kuwa suala la michezo limekuwa sehemu ya mipango yake ambapo katika kipindi cha kuanzia mwaka 2020 hadi sasa ameweza kutumia kiasi cha shilingi milioni 11 kutoka mfuko wa jimbo kuinua michezo kwa kununua vifaa vya michezo na kuanzisha mashindano mbalimbali.
Kwa upande wake Katibu wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa Oganaizesheni, Issa Gavu Akizungumza kwenye mkutano huo kwa niaba ya Kaimu Katibu Mkuu wa CCM, Anamringi Macha alisema kuwa wabunge wanaofanya kazi nzuri kama alivyofanya Dk.Samizi wanapaswa kulindwa na kupewa muda wa kutosha kufanya shughuli za maendeleo.
Gavu alisema kuwa wabunge na viongozi waliopo madarakani wako hapo kwa baraza za CCM hivyo chama hakitakubali kuona viongozi wenye nia ya dhati ya kuwaletea maendeleo wananchi na kusimamia maelekezo ya serikali wakisumbuliwa na watu wenye nia na uroho wa madaraka.
0 Comments