Na Mwandishi wetu
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imetia saini mkataba na taasisi nyingine za serikali wa ushirikiano katika udhibiti wa uchepushwaji wa kemikali bashirifu na dawa tiba zenye asili ya kulevya, lengo likiwa ni kukabiliana na biashara haramu ya kemikali hatari.
Mkataba huo ni kati ya DCEA na Mamlaka ya Maabara ya Kemikali ya Serikali (GCLA), Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba ya Tanzania (TMDA), Baraza la Famasi la Bohari Kuu ya Dawa (MSD) na wawakilishi kutoka sekta binafsi katika viwanda vya kemikali na dawa tiba zenye asili ya kulevya juzi jijini Arusha.
Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo alisema kichocheo kikuu cha kuimarisha juhudi hizi za pamoja kupitia mkataba huo wa ushirikiano ni, uwepo wa viashiria vinavyoonyesha ongezeko la biashara haramu ya kemikali hatari na matumizi yake katika uzalishaji wa dawa za kulevya na dawa mbadala za kulevya.
"Mkataba huu wa ushirikiano tunaangalia sehemu zenye uchepushwaji mkubwa wa dawa, tulishafanya kwa wadau wa Dar es Salaam, leo tumekutana hapa Arusha na tutaangalia miji mingine yenye tatizo kama hili nako tutafanya na baadaye tutaunda umoja wa wauzaji wa kemikali bashirifu na famasi zenye kibali cha kuuza dawa tiba zenye asili ya kulevya,”alisema na kuongeza.
"Ili kuhakikisha tunawekeana utaratibu wa ufuatiliaji wa karibu, tushirikiane kwenye kuzuia uchepushwaji wa kemikali bashirifu na dawa tiba zenye asili ya kulevya, "alisema Kamishna Lyimo.
Naye Meneja Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Kanda ya Kaskazini, Eliamni Mkenga alisema maabara hiyo ni miongoni mwa wadau muhimu wa DCEA kwa kuwa wanashirikiana nao kwa kiasi kikubwa udhibiti wa uchepushwaji wa kemikali bashirifu na udhibiti wa dawa zingine za kulevya.
“Kwenye dawa za kulevya kuna makundi mawili makuuu tunayoshirikiana na Mamlaka, Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imefanya kazi ya uchunguzi wa dawa za kulevya ikisaidiana na polisi pamoja na kitengo maalumu cha udhibiti wa dawa za kulevya,” alisema.
"Lakini baada ya kuanzishwa DCEA tunashirikiana nao katika kutambua aina za dawa za kulevya na kupima watumiaji kujua aina ya dawa za kulevya wanazotumia. Pili Maabara ya mkemia Mkuu wa Serikali inaangalia kemikali bashirifu na kwa kawaida inabidi kila mwezi tuwe na wasilisha ni kemikali gani zinapatikana nchini lakini mwisho kabisa tunatoa ushahidi mahakamani kwa kitaalamu katika kesi mbalimbali,’’ alisema Mkenga.
Kwa upande wake Meneja wa TMDA, Kanda ya Kaskazini, Proches Patrick alisema watatoa ushirikiano mzuri kwa mamlaka na taasisi zote zilizoingia makubaliano ya ushirikiano huo.
Aidha TMDA itaendelea kushirikiana na DCEA pamoja na taasisi zote ambazo zimeingia kwenye mkataba huo watahakikisha wanashirikiana na utekelezaji wake unakuwa na tija.
Mkataba huo wa ushirikiano unawakilisha hatua muhimu katika jitihada za kudhibiti kuenea kwa vitu hatari nchini Tanzania kinyume cha sheria.
Mwisho
0 Comments