Na Hamida Ramadhan,Matukio Daima App Dodoma
SEKTA ya Madini Nchini imevuka lengo la kuchangia asilimia 10 kwenye Pato la Taifa mwaka mmoja kabla ya muda uliopangwa kwenye Sera ya Madini ya 2009 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2021/22–2025/26.
Akizungumza jijini Dodoma, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amesema mchango wa sekta hiyo umefikia asilimia 10.1 mwaka 2024. "Hili ni matokeo ya sera bora, usimamizi makini na uwekezaji katika madini mkakati, uongezaji thamani na utafiti wa kina wa kijiolojia," amesema.
Mapato ya Serikali kutoka sekta hiyo yameongezeka kwa asilimia 20.8, kutoka sh. bilioni 623 mwaka 2021/22 hadi bilioni 753 mwaka 2023/24.
Sekta hiyo pia imechangia kwa kiasi kikubwa fedha za kigeni, ambapo mauzo ya madini nje ya nchi yaliongezeka kutoka dola bilioni 3.1 mwaka 2021 hadi bilioni 3.55 mwaka 2023. Kwa bidhaa zisizo asilia, mchango wa madini ulifikia asilimia 56.2 mwaka 2023, kutoka asilimia 53.8 mwaka 2021.
Kuhusu ajira, kampuni za uchimbaji madini ziliunda nafasi 19,356, ambapo asilimia 97.4 ya ajira hizo ni kwa Watanzania. Zaidi ya dola bilioni 3.5 kati ya bilioni 3.9 za bidhaa na huduma zilizonunuliwa migodini zilitolewa na kampuni za Kitanzania.
Hata hivyo Waziri Mavunde amesisitiza kuwa mafanikio hayo yanatokana na uongozi madhubuti wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na dhamira ya Serikali kukuza uchumi kupitia sekta ya madini.
0 Comments