NA MWANDISHI WETU,ZANZIBAR
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussen Ali Mwinyi amewaasa Viongozi wa Dini nchini Kuendelea kufundisha na kusimamia Maadili kwa Vijana pamoja na kukemea maovu ili kuwa na taifa lenye kufuata misingi iliyo mema.
Rais Dkt Mwinyi ametoa wito huo wakati akihutubia mamia ya Waumini wa Dini ya Kiislamu katika Hafla ya kumbukizi ya Miaka 100 ya Kifo cha Sheikh Omar Kullatein iliyofanyika katika Msikiti wa Ijumaa wa Malindi Mjini Zanzibar.
Sheikh Sayd Omar Kullatein ni miongoni mwa mwanazuoni maarufu katika bara la Afrika na Asia aliezaliwa Zanzibar ambapo katika uhai wake alifundisha Dini ya Kiislamu katika Nchi mbalimbali.
Dkt Mwinyi amesema ni vyema kwa Viongozi wa Dini kufundisha na Kusimamia Maadili kwa Vijana ili kuwa na kizazi kilicho bora.
"Tumeambiwa hapa Sheikh Omar Kullatein alikuwa ni mwanazuoni alisifika kwa tabia njema hivyo napenda kutoa wito kwa Masheikh na viongozi wa Dini kuendelea kufundisha vijana wetu tabia njema ili kuwa taifa lenye maadili,"amesema.
Aidha Dkt Mwinyi amewataka Viongozi wa Dini kuendelea kuhubiri Amani, Umoja na Mshikamano katika Taifa.
"Napenda kutoa wito kwenu kuendelea kuhubiri Amani,Umoja na Mshikamano ili kuchochea Uchumi na maendeleo endelevu," ameeleza.
Mapema akisoma historia ya Sheikh Omar Kullatein, Sheikh Mudhihirddin Bin Ali amesema Sheikh Omar Kullatein alikuwa kiigizo chema kwa tabia njema alizokuwa nazo wakati wa uhai wake.
Amesema, Sheikh Omar Kullatein katika kipindi cha uhai wake alitumia muda mwingi kutafuta kusoma elimu ya Dini ya Kiislamu katika Nchi ya Yemen, Zanzibar na Somalia.
"Sheikh Omar Kullatein alikuwa mwanazuoni ambaye muda mwingi alikuwa anafundisha Dini katika mataifa mbalimbali," ameeleza.
Katika Kumbukizi hiyo ya Miaka 100 ya Sheikh Omar Kullatein imehudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Serikali, Taasisi Binafsi, Masheikh, Wahadhiri wa Vyuo na Wanazuoni wa Kitaifa na kimataifa ambapo Dua, Khitma na Qaswida zilizimwa.
0 Comments