Header Ads Widget

WADAU WAPINGA KUFUNGWA SHUGHULI ZA UVUVI ZIWA TANGANYIKA

 



Na Fadhili Abdallah,Kigoma



CHAMA cha NCCR Mageuzi kimeitaka Serikali kusimamisha mpango wake wa kusimamisha shughuli za uvuvi katika ziwa Tanganyika kwa miezi mitatu vingenevyo itafungua kesi mahakamani kusimamisha utekelezaji wa mpango huo.


Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kigoma kuhusiana na uamuzi huo wa serikali unaotarajia kuanza kutekelezwa Mei 15 mwaka huu Katibu Mwenezi wa Chama Cha NCCR – Mageuzi Taifa,Frank Ruhasha alisema kuwa utekelezaji wa mpango huo unakwenda kinyume na sheria za uvuvi hivyo serikali ipitie upya mkataba wa LATAFIMA

na kanuni zake  kabla kuanza kwa utekelezaji huo ambao ni wa kimataifa lakini unakiuka sheria ya uvuvi.

 

Ruhasha alisema kuwa kama serikali itatekeleza mpango wanatarajia kwenda mahakamani kusimamisha mpango huo na kutoa wiki moja kwa serikali kupitia wizara ya mifugo na uvuvi kusimamisha utekelezaji wake na kwamba vinginevyo wataandaa maandamano kupinga jambo hilo.

 


Katibu huyo Mwenezi wa NCCR – Mageuzi alisema kuwa karibu watu milioni moja wanategemea shughuli za uvuvi katika ziwa Tanganyika kama njia kuu ya kujipatia kipato kwa ajili ya maisha yao ya kila siku lakini pamoja na hivyo serikali inafunga shughuli hizo huku kukiwa hakuna njia mbadala ya watu hao kwa ajili ya kujiingizia kipato.



Kwa upande wao wadau wa uvuvi mkoani Kigoma wameitaka serikali kutafakari upya mpango wa kufunga shughuli za uvuvi katika ziwa Tanganyika kwani kutekelezwa kwa mpango huo kutaathiri maisha ya wananchi wa mkoa huo ambao wanategemea uvuvi kama shughuli yao kuu ya kuwaingizia kipato.

 


Wakizungumza kwa nyakati tofauti wadau hao walisema kuwa mpango wa kufunga shughuli za uvuvi ambao ulitangazwa kuanza Mei 15 mwaka huu unapaswa ufanyiwe tathmini ya kina kabla ya kuanza kutekelezwa ili kubaini athari kubwa zitakazojitokeza kwa miezi mitatu ambayo shughuli hizo zitakuwa zimefungwa.



Mwenyekiti wa chama cha wavuvi manispaa ya Kigoma Ujiji, Ally Kibore alisema kuwa moja ya mambo ambayo wanapinga kutekelezwa kwa mpango huo ni Kanuni zilizowekwa na Mamlaka ya usimamizi ya ziwa Tanganyika (LTA) kupitia mradi wa maendeleo ya uvuvi ziwa Tanganyika (LATAFIMA) ambazo zinakwenda tofauti na sheria na kanuni za uvuvi nchini.


Kibore alisema kuwa pamoja na tofauti hiyo ya kanuni ambazo zinapingana na sheria za uvuvi nchini lakini pia changamoto kubwa ni uvuvi haramu ambao ndiyo unaochangia kuua mazalia ya samaki na kuvua samaki wachanga lakini bado changamoto hiyo wasimamizi wa uvuvi wameshindwa kufanyia kazi.


Kwa upande kiongozi wa wavuvi mwalo wa KGODECO, Ambatanisye Mwakalambile  alisema kuwa hawakubaliani na mpango wa serikali wa kufunga shughuli za uvuvi kwa kutumia kanuni za LATAFIMA wakati wizara inayo sheria na kanuni zake ziko vizuri lakini zimekosa usimamizi hivyo wanapingana bna mpango huo badala yake wasimamie sheria na kanuni za uvuvi za nchi.


Mmoja wa wavuvi wa ziwa Tanganyika kutoka Mwalo wa Katonga manispaa ya Kigoma Ujiji,Juma Yahaya alisema kuwa mpango wa serikali kufunga shughuli za uvuvi ziwa Tanganyika ni kilio kikubwa kwao na hasa kutekeleza kwa kutumia kanuni za mradi badala ya kutumia sheria na kanuni za nchi ambazo zinapingana kwenye taratibu mbalimbali.




Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI