Header Ads Widget

JUMUIYA YA WAZAZI MABATINI WAADHIMISHA WIKI YA WAZAZI KITAIFA



NA CHAUSIKU SAID _ MATUKIO DAIMAAPP MWANZA.


Jumuiya ya wazazi kata ya mabatini wilaya ya nyamagana Mkoani Mwanza wameadhimisha wiki ya wazazi Kitaifa Kwa kutoa elimu ya Mmomonyoko wa maadili katika shule ya sekondari Mtoni.


Akizungumza katika maadhimisho hayo Katibu wa Jumuiya ya wazazi wa kata hiyo Haji Said ameeleza kuwa wameamua kutoa elimu hiyo kutokana na vijana wengi kuiga utamaduni wa kigeni hali inayopelekea kuwa na Taifa lisilo na maadili mema.



Said amesema kuwa jamii inapaswa kuwasimamia watoto Kwa ukaribu ili kukomesha mmomonyoko wa maadili na vitendo vya ukatili Kwa kushirikiana na walimu Kwa ukaribu.


"Yale tunayoyaiga ndio yanasababisha Mmomonyoko wa maadili, Kuna msemo unasema mkataa kwao ni mtumwa na sisi tunaona tunataka kuwa watumwa na ndio maana tumeamua kukutana hapa ili kuweza kujadili usalama wa familia zetu" Alisema Said.



Inspector Kagemlo Muhula, Mkuu wa dawati la jinsia na watoto kituo cha polisi Wilaya ya Nyamagana Amesema kuwa Mmomonyoko wa maadili unasababishwa na wazazi kushindwa kutimiza wajibu wao katika swala la malezi na makuzi Kwa watoto.


"Watoto wanaachiwa kujilea wenyewe wazazi wanakuwa na visingizio vya kutafuta maisha na kushindwa kuangalia mwenendo wa tabaia za watoto wao" Alisema Muhula.



Muhula Amesema kuwa jamii inapaswa kuendelea kuripoti vitendo viovu vinavyotendeka ndani ya jamii na kuachana na kuwa na hofu ya kuripoti matukio hayo ili serikali kuendelea kuchukua hatua Kwa wahusika.


Kwa upande mwingine ameeleza kuwa mahakama inapaswa kufanya kazi Kwa uweledi na waendesha mashtaka kushirikiana na jeshi la polisi kuhakikisha watuhumiwa wanapewa stahiki zao kutokana na makosa wanayoyafanya ndipo matukio haya yatapungua.



" Wakati mwingine inakatisha tamaa sana kama mmemkamata mtuhumiwa na kesi imeendaa Kwa mwanasheria na shitaka limetoka kesi imeendaa mahakamani unashangaa mtuhumiwa anaachiwa na unaamini ushahidi wako umekamilika na kazi imefanyika vizuri" Alisema Muhula.


Muhula ameitaka jamii kuendelea kuripoti ukatili na sio kuufumbia macho na kukaa kimya ni lazima watoto waendeleekuwa salama na Taifa Kwa ujumla



Joseph Mukoji Mratibu wa sheria Utetezi na Uzingatiaji kutoka Wote Sawa ameeleza kuwa swala la Mmomonyoko wa maadili sheria maalumu ya Mtoto iliyotungwa mwaka 2009 inasimamia Msingi wa ufatiliaji Kwa Mtoto kuzuia ajira hatarishi pamoja na malezi stahiki.


Mukoji amefafanua kuwa utoaji wa Taarifa ni muhimu katika kufichua vitendo vyote viovu hususani vinavyosababisha Mmomonyoko wa maadili.


" Kama ukatili unafanyika lazima vitendo viripotiwe, bahati mbaya siku hizi tumekuwa na jamii ambayo inaweza kushuhudia vitendo vinavyofanyika kinyume na Sheria na Taratibu za Nchi na wasiripoti na kuona kama ukatili huo hauwahusu" Alisema Mukoji.


Aidha ameeleza kuwa Kila mmoja anawajibu wa kupunguza vitendo vya ukatili na Mmomonyoko wa maadili na makosa mbalimbali Kwa kufata sheria na Taratibu za Nchi.



Katibu Elimu Malezi na Mazingira Magabe Mahelesi Amesema kuwa wazazi wamesahau majukumu yao juu ya watoto na kutumia muda mwingi katika shughuli zao na kusababisha watoto kuingia katika vitendo viovu.


"Muda mwingi watoto wanajilea peke yao na sisi tumesahau majukumu yetu yanayotupasa Kwa watoto wetu hali inayopelekea watoto kujipangia majukumu wenyewe" Alisema Mahelesi.


Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Mtoni Titi Mwendwa amefafanua kuwa Mmomonyoko wa maadili unaanzia Kwa watoto kutokana na kukosa ukaribu kutoka Kwa wazazi wake.



Mwendwa Amesema kuwa wazazi wanalo jukumu la kukaaa na kuongea na watoto wao Kwa ukaribu ili watoto wapate nafasi ya kuzungumza waliyonayo na sio kuwaacha wajilee peke yao.


"Sisi walimu tumekuwa tukikemea vitendo hivyo viovu Kwa kufata sheria na taratibu za shule ili wanafunzi waweze kuishi Kwa kufata maadili" Alisema Mwendwa.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI