NA WILLIUM PAUL, SIHA.
MKUU wa wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, Thomas Apson amefanya ziara kujionea ujenzi miradi mbalimbali ya sekta ya Elimu na Afya ambayo inatekelezwa na Serikali ya awamu ya sita.
Apson ameridhishwa na ujenzi wa miradi hiyo na kutumia nafasi hiyo kumpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Pendo Mangali pamoja na watumishi wa Serikali kwa jinsi ambavyo wanasimamia fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya maendeleo ya wilaya ya Siha.
"Mkurugenzi pamoja na timu yako mnanifanya nijisikie mwenye bahati sana kufanya kazi na watu wa aina yenu mmekuwa mstari wa mbele kuhakikisha fedha zinazoletwa na Serikali zinatumika kama zilivyokusudiwa" alisema Apson.
Alisema kuwa, Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hasani imejikita katika kutatua kero na matatizo mbalimbali yanayowakabili wananchi na ndio maana imemwaga fedha nyingi kwa wilaya ya Siha.
Watumishi hao walimweleza Mkuu huyo wa wilaya kuwa moja ya changamoto wanazokumbana nazo katika ujenzi wa miradi hiyo ni maji ya kutumika katika ujenzi kutokana na ukame unaoendelea kuwepo.
Walisema kuwa, ili kukabiliana na changamoto hiyo katika shule Sekondari ya Karansi inayopelekea kasi ya ujenzi kupungua hali iliwalazimu kuchimba kisima cha maji ya chini kupata maji ya uhakika ili ujenzi wa madarasa matatu pamoja na nyumba ya walimu wawili katika nyumba moja shuleni hapo unakamilika.
Mkuu huyo wa wilaya aliagiza kuongezeka kwa nguvu kazi katika uchimbaji wa kisima hicho ili kuufupisha muda wa kukichimba ili kazi ya ujenzi iendelee na kutumia nafasi hiyo kuwapongeza wananchi kwa kujitolea nguvu kazi kuchimba msingi.
Aidha alisema kuwa, ipo changamoto ya aina ya udongo kwenye baadhi ya maeneo katika kumwaga jamvi imara ambapo imeonekana katika shule ya msingi Matadi kata ya Ndumeti pamoja na na nyumba ya watumishi wawili katika nyumba moja zahanati ya Mwangaza kata ya Ngarenairobi.
"Ujenzi wa floor na stability ya majengo katika maeneo hayo unataka umakini sana kiasi cha kwamba kote majengo imebidi yawe na lenta tatu, pale Matadi mafundi wamekuwa wajanja kwa kuamua watumie movements za mafundi na vibarua kupandisha ukuta na kuweka lenta huku wakiimarisha sakafu ya udongo iliyopo kabla ya kumwaga jamvi kwa kushindilia udongo kila watembeapo" alisema Apson.
Aidha shule ya msingi ya Matadi alifurahishwa sana kuona matumizi ya tofali za kiwanda cha Halmashauri maana hiyo itatupunguzia gharama za ujenzi.
"Fundi wa ujenzi wa nyumba ya 2 in 1 ya Mwangaza amenidokeza kuwa namna bora ya kuwa na jamvi imara ni kutumia aina fulani ya Wire Mesh yenye matundu mapana ambayo ndio inawekwa juu ya mawe ya msingi na baadae lile rojo la cement hufanya jamvi lake kuwa imara kabisa" alisema Apson.













0 Comments