Header Ads Widget

TMA YATOA TAARIFA YA MWENENDO WA HALI YA KLIMATOLOJIA

 


Na Fatma Ally MDTV Dar es Salaam


MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa taarifa rasmi ya Mwenendo wa Hali ya Klimatolojia ilivyokuwa kwa mwaka 2021, ambapo imeeleza kuwa ilikuwa na hali mbaya iliyoambatana na madhara kwa baadhi ya maeneo.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam,mara baada ya kutoa taarifa hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Agnes Kijazi amesema kwa mwaka 2021 Tanzania ilikumbwa na matukio ya hali mbaya ya hewa hususan mvua kubwa zilizoambatana na mafuriko na upungufu wa mvua pia katika baadhi ya maeneo, joto pamoja na upepo mkali.


"Mwaka wa 2021, nchi yetu ilikumbwa na matukio ya hali mbaya ya hewa hususan mvua kubwa zilizoambatana na mafurikona upungufu wa mvua katika baadhi ya maeneo, joto pamoja na upepo mkali ambapo ameneo mengi yaliathiriwa na mafuriko ikiwa ni pamoja na mikoa ya kusini na magharibi mwa nchi ambapo yalisababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu ikiwemo barabara na madaraja, makazi, na mashamba," amesema Dkt. Kijazi.


Amesema kuwa, January 12, 2021 Mvua kubwa ya milimita 369.7 ilinyesha Mtwara na kuvunja rekodi ya mvua iliyowahi kupimwa ndani ya saa 24 katika Kituo cha hali ya hewa cha Mtwara tangu kuanzishwa kwake mwaka 1951.


Hata hivyo, amesema , mvua ya mawe iliyoleta taharuki ilinyesha wilayani Biharamulo Agosti 14 2021, kipindi ambacho kawaida huwa hakina mvua kwa maeneo hayo.


Ameongeza kuwa, kipindi cha ukavu cha muda mrefu kilitokea katika miezi ya Oktoba na Disemba 2021 na kusababisha athari kubwa kwa jamii na uchumi hasa jamii za wafugaji ambapo idadi kubwa ya mifugo ilikufa kwa njaa na kukosa maji katika baadhi ya maeneo ya mikoaya Arusha, Kilimanjaro, Morogoro, Manyara na Pwani.


Amesema kuwa, kutokana na changamoto hizo za hali ya hewa ambazo zimekuwa zikijirudia mara kwa mara, mamlaka imejikita kufanya uchambuzi wa kina wa hali ya hewa kila mwaka na kisha kutoa ripoti ya hali ya Klimatolojia kwa mwaka husika.


Aidha, ripoti hiyo inatoa taarifa za kina kuhusu matukio ya hali mbaya ya hewa yaliyotokea na madhara yake katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na pia hubainisha ukubwa wa matukio haya kwa kulinganisha na matukio ya namna hiyo yaliyotokea miaka iliyopita.


Aidha, amewakumbusha  wataalam katika sekta mbalimbali kufuatilia taarifa mpya ya tathmini ya mabadiliko ya hali ya hewa kuhusiana na athari na uhimilivu wa mabadiliko ya hali ya hewa iliyotolewa  Februari 28,2022 na Jopo la Kiserikali la Tathmini ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC).

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI