Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima App Dodoma
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imesema wateja wake wa leseni hawalazimiki tena kufika katika ofisi za mamlaka hiyo kupata huduma, kwani sasa huduma zote zinapatikana mtandaoni kupitia mifumo ya kidijitali, hatua iliyolenga kupunguza usumbufu kwa wananchi na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma.
Akizungumza katika maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika viwanja vya Chinangali, jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dkt. James Andilile, alisema kuwa maboresho ya mifumo ya TEHAMA yamewezesha wananchi kupata huduma wakiwa mahali popote nchini, bila kulazimika kufika katika ofisi za kanda sita za mamlaka hiyo.
“Tumejipanga kuhakikisha wananchi hawapotezi muda kusafiri kwenda ofisi za EWURA. Kupitia mifumo yetu ya kidijitali, huduma zote muhimu sasa zinapatikana kwa njia ya mtandao. Tutaendelea kuboresha mifumo hii ili iende sambamba na mahitaji ya sasa na kaulimbiu ya serikali ya kuimarisha uwajibikaji,” alisema Dkt. Andilile.
Ameongeza kuwa EWURA, kama chombo cha udhibiti wa huduma muhimu kama maji, umeme, mafuta na gesi asilia, inasisitiza uwazi kwa taasisi zote inazozisimamia kwa kuzitaka kuweka mikataba ya huduma kwa wateja kwenye tovuti zao rasmi, ili kuwezesha wananchi kujua haki na wajibu wao kuhusu huduma hizo.
“Ukihusika na sekta ya maji, hakikisha taarifa za huduma zako na haki za wateja zinaonekana wazi. Hii itasaidia wananchi kuwa na uelewa sahihi juu ya kile wanachopaswa kupata, na wapi wakatoe malalamiko pindi wanapohisi haki zao zinavunjwa,” alieleza.
Aidha, Dkt. Andilile alitumia fursa hiyo kuonya baadhi ya vituo vya mafuta vinavyouza bidhaa hiyo kwa bei ya juu kinyume na bei elekezi iliyotangazwa na EWURA. Alisema bei ya mafuta ya petroli kwa sasa ni Sh 2,905 kwa lita, lakini kuna taarifa za baadhi ya vituo kuuza hadi Sh 5,000, jambo ambalo ni ukiukwaji wa sheria.
“Tunatoa wito kwa wananchi wanaokumbwa na hali hii kupiga simu ya bure 0800110030 ili kutoa taarifa. Kituo chochote kitakachobainika kuuza mafuta kwa bei ya juu kuliko iliyowekwa na EWURA kitachukuliwa hatua kali, ikiwemo kufutiwa leseni,” alisisitiza.
Mkurugenzi huyo alieleza kuwa maonesho hayo ni fursa ya kipekee kwa wananchi kupata huduma moja kwa moja kutoka kwa taasisi mbalimbali za serikali, huku akibainisha kuwa EWURA imepeleka mifumo yote ya utoaji huduma kwenye banda lake, ili wananchi wapate huduma papo kwa papo.
EWURA ni miongoni mwa taasisi za serikali zinazoshiriki katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwa mwaka 2025, ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali kuboresha uwajibikaji na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Mwisho
0 Comments