Header Ads Widget

PROF.MKENDA AIPONGEZA TET KWA TUZO ZA STADI ZA KUFUNDISHIA NA UJIFUNZAJI KWA WALIMU NCHINI

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda akipokea tuzo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dkt. Aneth Komba 


Na. Andrew Chale, Matukio Daima App Dar.


WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda ameipongeza Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kwa kusimama imara katika kutekeleza majukumu yake ikiwemo usimamizi na uendelezaji wa Tuzo za Stadi za Kufundishia na Ujifunzaji kwa Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari nchini.

Waziri Prof. Mkenda ameyasema hayo jana Jumamosi Jioni Julai 14, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya utoaji tuzo hizo kwa msimu wa tatu zenye lengo la kuchochea walimu kuwa wabunifu kwa kutumia mbinu shirikishi za ufundishaji tukio lililofanyika katika ukumbi wa Maktaba mpya ya Chuo Kikuu Dar Es Salaam (UDSM).

“Wakati tunaanza tulianza na Walimu wa Shule za Msingi, lakini nashukuru mkajiongeza na sasa mmeongeza na wa Sekondari hayo ni mafanikio makubwa na ninawapongeza kwani hamjawahi kutuangusha,” amesema Prof.Mkenda.



Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda akizungumza katika tukio hilo 


Prof. Mkenda ameongeza kuwa ndio maana wanatoa tuzo hizo kwa kuwa wanathamini mchango wa walimu kutokana na kazi kubwa wanayoifanya kufunza vijana, kuwalea na kuwajenga katika misingi bora.

Aidha, ametoa maelekezo kwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Carolyne Nombo kupanga bajeti ya kuendesha Tuzo hizo ili ziwe za kudumu.

“Hili jambo la kutoa tuzo ni zuri na linafanyika kwa kuwa linadhaminiwa na Benki ya Dunia (WB), hivyo nasi tuanze kuandaa bajeti ili ziwe za kudumu, sasa Katibu Mkuu katika vikao vyenu hakikisheni mnaandaa bajeti ya tuzo hizi, ingawa (WB) bado tunawahitaji,” amesema Prof. Mkenda.

Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dkt. Aneth Komba


Kwa upande wake, Mkurugenzi  Mkuu wa TET, Dkt. Aneth Komba amesema tuzo hizo zinatoa fursa kwa walimu kuonesha umahiri wao wa kufundisha kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), kwani inamsaidia mwanafunzi kufanya vizuri katika maisha baada ya kuhitimu masomo yake.

Ameongeza kuwa shindano hilo lina lengo la kutoa fursa kwa walimu wa somo la Sayansi, Shule za Msingi na Hisabati na Sayansi kwa kidato cha kwanza kuonesha umahiri wao wa kutumia Tehama na mbinu shirikishi katika ufundishaji ili kuleta chachu katika kukuza Stadi ya Karne ya 21.

Ameongeza kuwa katika kuwapata washindi, walimu walituma video zao walizojirekodi wakiwa wanafundisha na zilichujwa kuanzia ngazi za Halmashauri hadi Taifa kupitia wataalamu wenye sifa na kufanikisha kupatikana washindi.

“Changamoto kubwa ambayo tumeipata ni baadhi ya walimu kurekodi maudhui ambayo yapo nje ya makusudio, tunawaomba katika msimu ujao wazingatie kinachohitajika na washiriki,” amesema.

Pia aliishukuru WB Kwa kuendelea kudhamini shindano hilo kupitia miradi ya Boost na Sequip inayokusudia kuongeza uwezo wa Walimu katika nyanja ya ufundishaji na ujifunzaji kupitia mafunzo endelevu Kwa walimu kazini (MEWAKA).

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkazi wa benki ya Dunia, Bi. Gema Toddy aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkazi wa benki hiyo Nathan Belete


Kwa upande wake, Gema Toddy ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Nathan Belete amesema wanafadhili miradi mbalimbali ya elimu hapa nchini na kufafanua kuwa ili kuwa na elimu bora ni lazima mwalimu awe bora na ndio sababu iliyowasukuma kufadhili tuzo hizo.

“Wakati tunaanza kudhamini tuzo hizi, tulianza na Walimu wa Shule za Msingi na sasa tumeongeza wigo hadi Sekondari, lengo letu ni kuhakikisha kunakuwa na walimu bora watakasaidia kuwa na elimu bora na kutengeneza wanafunzi bora,” amesema.




Katika hafla hiyo, mshindi namba 10 hadi 4 kwa masomo ya Fizikia, Kemia, Hisabati, Biolojia na Sayansi walipatiwa vyeti na washindi wa tatu walijinyakulia kitita cha Sh.Milioni 2.5, wa pili Milioni 3/- na washindi wa kwanza walijizolea kitita cha Sh.Milioni 4/-

Walimu wa shule za msingi waliojinyakulia nafasi ya tatu katika shindano hilo kwa msimu huu ni Mwalimu wa Shule ya Msingi Ntandi, Haji Mohamed, Mwalimu Theresia Rogath wa Shule ya Msingi Sombetini Arusha na Mwalimu Teleza Boniphace wa Shule ya Msingi Mahina Mwanza.

Walioshika nafasi ya tatu kwa upande wa Sekondari ni Halfani Hamisi wa Chidy Sec iliyopo Masasi mkoani Mtwara (Fizikia), Kleruu Sumaye wa Shule ya Sekondari Mringa iliyopo mkoani Arusha (Kemia), Hongera Nguvile wa Shule ya Sekondari ya wasichana Buseke(Hisabati) na Zakaria Bujingwa wa Shule ya Sekondari Mkata Handeni Tanga.




Walioshika nafasi ya pili ni Jema Mkonongo wa Sekondari ya Tandale (Dar es salaam), Neema Diliwa wa Sekondari ya Makumbusho (Kinondoni Dar es salaam), Emmanuel Mkama wa Melela Sekondari (Morogoro) na Athur Simkonde.

Walioshika nafasi ya kwanza ni King Kigongo wa shule ya Msingi Nassoro Seif (Morogoro), John Patrick wa Sekondari ya Muungano ya Usariver Arusha, Peter Lymo wa Sekondari ya Kilangale (Same Kilimanjaro) na Samuel Adriano wa Sekondari ya Madibira ya Mbeya.










Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI