Na Mwandishi Wetu_ Muleba.
Mkuu wa Wilaya ya Muleba Toba Nguvila amewaasa timu ya vijana wa Azam walio na umri wa chini ya miaka 20 kuendelea kucheza mpira kwa viwango, ili kukuza vipaji vyao, na kuweza kupata ajira ndani na nje ya nchi.
Akizungumza na vijana wa timu hiyo waliotembelea wilayani Muleba kwa lengo la kusaka vipaji, Mkuu huyo wa Wilaya amesema kuwa mpira wa sasa ni ajira hivyo vijana wote wenye vipaji vya kucheza mpira waviendeleze kwa manufaa yao, jamii inayowazunguka na taifa kwa ujumla.
"Tunahitaji akina Messi, Zidane, Samuel Etoo na kina Drogba wengi, na hata akina Msuva na Mbwana Samatta ambao ni wa Tanzania wapo wanacheza timu za nje ya nchi na kuitangaza Tanzania kimataifa" amesema Nguvila.
Pia, amewasihi vijana hao kutumia vipaji vyao kujiendeleza zaidi, ili kupitia kucheza mpira waweze kuwa makocha wa kuongoza timu mbalimbali za michezo hapa nchini na kusaidia kupata waamuzi vijana wenye uwezo wa kusimamia na kukimbia kwa spidi kuangalia makosa yanayotokea uwanjani wakati wa mechi, ili kuondoa changamoto za timu kupata pointi isivyo kihalali.
Aidha amempongeza mwekezaji Said Salim Bakhresa kwa kuwekeza katika michezo, kwani ameweza kuikuza tasnia ya michezo Tanzania, kuongeza mashabiki wa mpira wa miguu pamoja na mashabiki wa michezo mbalimbali wanaoangalia michezo ya ndani ya nchi pamoja na ligi za kimataifa, kupitia king'amuzi cha Azam.
"Naipongeza pia timu ya vijana ya Azam kwa kuja Muleba, na nawaahidi kuendelea kuwa shabiki wa Azam Sport Academy na Azam Sports Club, na nawahakikishia kuwa hapa wilayani Muleba mtakuwa salama na hakuna mtu ambaye atapata tatizo mpaka shughuli iliyowaleta itakapokamilika" amesema Nguvila.
Kwa upande wake Afisa Utamaduni wa Halmashauri ya wilaya ya Muleba, Denis Joseph amesema kuwa timu hiyo imefika wilayani hapo kwa lengo la kutembelea kituo cha michezo kilichopo kata ya Nshamba kinachojulikana kama Muleba Youth Academy, kwa lengo la kutambua vipaji vilivyoko katika wilaya ya Muleba na Mkoa wa Kagera kwa ujumla.
Denis amesema kuwa timu hiyo ya vijana walio chini ya umri wa miaka 20 watakuwepo Muleba mpaka tarehe 5 mwezi huu, na siku hiyo watacheza mchezo wa kirafiki kati ya timu ya vijana ya Azam na timu ya vijana ya Muleba Youth Academy kuanzia saa tisa mchana.
Wakizungumza baada ya kuwasili ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Muleba kwa lengo la kujitambulisha na kueleza madhumuni ya ziara yao, Kocha Mkuu wa timu ya Azam ya vijana chini ya miaka 20 Mussa Rashid Omari ameeleza kuwa lengo la ujio wao katika wilaya ya Muleba Mkoa wa Kagera ni kupata vipaji vipya, na kwamba utaratibu walionao hivi sasa ni kutembelea kwenye mikoa yote hasa mikoa ya pembezoni ya nchi kwa ajili ya kupata wachezaji wenye vipaji, ambao wataweza kuwaongeza kwenye timu yao ya vijana.
0 Comments