.
Na Amon Mtega,Songea.
MJUMBE wa kamati tendaji taifa wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) Sabina Lipukila amewataka Viongozi wa Mkoa wa Ruvuma wanao wakilisha Walimu kutoka kwenye maeneo yao kwenda kutatua changamoto za Walimu hao pamoja na kuwahimiza kupitishia mishahara yao kwenye benki ya mwalimu (MCB).
Wito huo ameutoa wakati akizungumza kwenye kikao cha baraza la Walimu hao kilichofanyika Mjini Songea Mkoani humo ambacho kilijadili mambo mbalimbali ikiwemo changamoto zinazo wakabili Walimu kwenye maeneo yao ya kazi ,huku baadhi ya wajumbe wa baraza hilo walichangia hoja mbalimbali.
Lipukila amesema kuwa kumekuwepo na changamoto nyingi kwa Walimu ikiwemo ya madai yao mbalimbali lakini zimekuwa hazitatuliwi kwa wakati jambo ambalo limekuwa likiwakatisha tamaa Walimu katika utendaji kazi wao .
Mjumbe huyo licha ya kuwataka Viongozi hao kwenda kutatua changamoto hizo lakini bado amewataka waende wakawaambie Walimu wote mishahara yao ipitie kwenye benki ya mwalimu ili kuikuza benki hiyo ambayo imeshakuwa na hisa za Walimu.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Chama Cha Walimu katika Manispaa ya Songea Emmanuel Komba akichangia hoja amesema kuwa kwa upande wa kutumia benki ya Mwalimu ameshatoa maelekezo kwa Walimu wake juu ya uzuri wa benki hiyo na kuwa tayari baadhi yao wameshaanza kuitumia huku malengo katika mwaka huu ni kuhakikisha Walimu wote wa Manispaa ya Songea wanatumia benki hiyo .
Komba amesema kuwa licha ya kuweka mikakati ya kuhakikisha Walimu wa Manispaa hiyo wanatumia benki hiyo lakini bado ameweza kutatua changamoto za baadhi ya Walimu hasa waliyokuwa wakidai madai mbalimbali.
Naye Hassan Said ambaye ni katibu wa Chama Cha Walimu Wilaya ya Nyasa amesema kuwa Walimu waliyowengi hawatambui haki za stahiki zao hasa pindi wanapopatiwa uhamisho kutoka kituo kituo ambacho anafanyia kazi kwenda kituo kingine cha kazi.
Hata hivyo katibu wa Chama Cha Walimu Mkoa wa Ruvuma Onesmo Makwembe amesema kuwa ofisi yake hakuna mtumishi anayedai malipo ya uhamisho kutoka Serikalini.
Akihitimisha kikao cha baraza hilo mwenyekiti wa Chama Cha Walimu Mkoa wa Ruvuma Kolimeje Kolimeje amewataka wajumbe hao kuzingatia maagizo waliyokubaliana ikiwemo na kuwaingiza wanachama wengi kwenye chama hicho.
Mwisho.
0 Comments