MAMLAKA za Maji nchini zimetakiwa kujadiliana na wadaiwa sugu namna gani watakavyolipa madeni yao na baada ya makubaliano wawarejeshee huduma ya maji kwa wale waliokatiwa.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Maji Juma Aweso kwenye Kijiji cha Msoga Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo baada ya ziara ya kamati ya Bunge ya Maji, Kilimo na Mifugo ilipotembelea kuona miradi ya Maji maeneo ya Mlandizi, Chamakweza na Msoga.
Aweso alisema kuwa wakurugenzi wa mamlaka za maji wakae na wadaiwa sugu ili wakubaliane na mamlaka na wasikatiwe maji ili walipe kidogo kidogo wanamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuiwezesha Wizara hatutakuwa kikwazo watu kupata maji.
Aidha amezitaka Mamlaka kuwaunganisha maji wateja wao ndani ya siku saba ili kuhakikisha huduma hiyo inapatikana kwa haraka na wakati.
Alisema kuwa wananchi wana ari ya kupata huduma ya maji na hawataki kusikia mtu anakaa miezi sita bila ya kuunganishiwa maji zisizidi siku saba kwani wanafanya jitihada hawataki kusikia eti viungo havipo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dk Christine Ishengoma alisema kuwa mambo yanakwenda vizuri jinsi mamalaka wanavyogawa maji yanakwenda hadi Morogoro kupitia mitambo ya Ruvu Juu na Ruvu Chini watu wa Morogoro na Pwani na Dar es Salaam watakuwa na huduma za uhakika.
Naye Mtendaji mkuu wa Dawasa Cyprian Luhemeja alisema kuwa kwa mradi wa Chamakweza utaenda hadi Morogoro ambapo hiyo ni hatua ya kwanza na ya pili itakuwa ni kusambaza kwa wananchi.
Naye mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Bagamoyo Abdul Sharifu alisema kuwa Chalinze na Bagamoyo kulikuwa na tatizo kubwa la maji na lilikuwa ni donda ndugu leo imekuwa historia kwani wananchi walikuwa wakilalamikia sana.
0 Comments