Header Ads Widget

JE DAMU HII INALIPWA NA NINI?



Adeladius Makwega-DODOMA


Machi 23 ya kila mwaka imeteuliwa kuwa ni siku ya maadhimisho ya Siku ya Ukombozi Kusini mwa Bara la Afrika, kwa Tanzania mwaka huu inafanyika huko Kongwa mkoani Dodoma kama ilivyonukuliwa na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Utamaduni nchini Dkt Emmanuel Temu.


”Kutakuwa na shughuli mbalimbali katika tukio hilo kwa heshima ya harakati za Ukombozi wa Barani Afrika kama vile mashindano ya insha na kazi kadhaa za sanaa.”


Kwa heshima ya kumbukumu hiyo na heshima ya roho kadhaa za Waafrika waliopambana na kufariki katika kulikomboa bara hili naomba nitumie siku ya leo kuyasimulia matukio mawili ya wapigania uhuru; Wakiwa nchini Tanzania na wakiwa uwanja wa mapigano.


Mwaka 2015 nikiwa Mtayarishaji Vipindi wa TBC Taifa nikitayarisha ripoti mojawapo ya Kipindi cha Habari na Muziki cha Shirika hilo kilichokuwa kinaruka hewani kila siku ya Jumatatu hadi Ijumaa Saa 12.00-1.00 Jioni, Fundi Mitambo wa TBC Taifa (tangu RTD)  Isaya Odinga ambaye leo hii ni marehemu aliniambia jambo.


“Nyinyi mnafanya mahojiano na watu wengi wa mbali, na wakubwa ambao mnadhani walishiriki kupigania uhuru, lakini mnatuacha siye tuliyofanya nao kazi kwa karibu mno wakati wa harakati hizo za ukombozi na yapo mengi tunayoyafahamu mengi hamuyatambui kabisa na hayapo hata katika maktaba yenu bali yapo ndani ya mashuhuda ambao ni sisi.”


Jambo hilo lilinigusa sana kwa hiyo siku iliyofuata ambayo ilikuwa ni siku ya uhuru wa Msumbiji Juni 25, 2015 nilimuhoji Fundi Mitambo Isaya Odinga juu ya harakati hizo za ukombozi.


Aliaza kwa kusema kuwa Wapigania Uhuru walitumia vizuri Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) na External Service (ES) kama chombo cha kuwafikishia ujumbe ndugu zao waliokuwa katika mataifa yao kupitia Ampitude Modulation (AM) na Short Wave (SW). 


Ndugu Odinga aliniambiwa kuwa kwa karibu wapigania uhuru walikuwa ni watu waliokuwa wakipambania haki zao, kwanza walianza katika mataifa yao na baadaye kuzihamishia harakati hizo katika mataifa mengine likiwamo Tanzania.


Wakiwa Tanzania walikuwa na changamoto kadhaa, kubwa lilikuwa ni matumizi ya lugha ambapo wengi walikuwa wakitumia lugha za kwao za asili na kidogo Kiingereza. Huku wengine waliweka juhudi za kuijfunza Kiswahili.


Fundi Mitambo huyu aliniambia kuwa kuna siku walikuwa wakirusha hewani kipindi kimojawapo chenye maudhui ya harakati za ukombozi na miongoni mwa waliopaswa kushiriki kipindi hicho aliyekuwa mpigania uhuru alichelewa kufika studioni.


Kipindi kilianza kwa waliowahi na ndugu huyu alipofika aliingia katika mlango wa studio husika na alipoambiwa matangazo yapo hewani alitaka kuingia kwa fujo. Wakati anataka kuingia alizuiliwa na walinzi wa RTD, jambo hilo lileta mgogoro mkubwa baina ya mpigania uhuru huyo na watumishi wa RTD.


Baadaye lilizungumzwa, mpigania uhuru kuelezwa utaratibu ulivyo wa studio na mwisho wa siku jambo hilo lilikaa sawa na dhana ya watumishi wa RTD kama walikwamisha harakati za ukombozi liliondoka kwa mpigania uhuru huyo.


Tukio lingine lilikuwa katika uwanja wa mapigano, desturi za mapambano ya kupigania uhuru ilikuwa mataifa kadhaa yalijumuika katika kulikomboa taifa lingine kwa dhana ile ya mwalimu Julius Nyerere, 


“Tanzania haiwezi kuwa huru kama mataifa mengine ya Afrika yakiwa chini ya mikono ya mabeberu.”


Wakiwa uwanja wa mapambano huko Msumbiji siku hiyo vita vilikuwa vigumu mno, kwani vikosi vya Frelimo vilishambuliwa mno na kusababisha wanamgambo kadhaa kupoteza maisha.

Hali hii haikuwakatisha tamaa wapigania uhuru wa Msumbiji na wenzao katika uwanja wa vita bali iliongeza ari ya vita kwa wachache waliosalia vitani waliokuwa mstari wa mbele.


Kiongozi mmojawapo katika vita hivyo akiwa na msaidizi wake waliomba msaada kwa wenzao waliokuwa nyuma ya uwanja wa vita baada ya kuwajulisha kilichotokea.


Ili kuwasubiri wenzao waje waliamua kuingia katika handaki mojawpao ambalo lilikuwa kando ya uwanja wa vita. Walipoingia ndani ya handaki hilo walikubaliana kuwa kwa usalama wao kila mmoja aingia katika handaki lake.


Kwa hiyo msaidizi wa kiongozi huyo alitoka katika handaki nambari moja na kuingia handaki nambari mbili.


Hali ilizidi kuwa mbaya huku maadui waliporomosha risasi na mizinga mizito katika eneo hilo. Sasa wakikaribia eneo walipojificha ndugu hawa wawili.


Wakiwa katika eneo hilo, walisogelea msitu mdogo na walikutana na handaki la kwanza wakaingia na mienge na tochi humo alipojificha kiongozi wa wapigania uhuru na hawakuweza kuona chochote.


Walingia katika handaki la pili, kama kawaida kwa mienge na tochi, kwanza hawakuona kitu, walirudi tena, ahmadi! walikutana na kigoda.Kigoda hicho ndicho kilikuwa kiti cha kiongozi wa wapigania uhuru akikalia wakati akizungumza na wapigania uhuru uwanja wa vita.


Kigoda hicho kilitoa picha kuwa hapo kuna watu, walikitoa nje na kuendelea kulikagua handaki hilo nambari mbili.


Kazi hiyo ilisababisha kumuona msaidizi wa kiongozi wa wapigania uhuru na kumtoa hadi nje ya handaki nambari mbili. Kwa kuwa handaki namba mbili lilikuwa kwenye kichaka walimbeba na kumpeleka eneo la wazi kidogo jirani na handaki nambari moja ambalo alikuwemo kiongozi wa wapigania uhuru.


Walipofika hapo walimketisha katika kigoda msaidizi wa kiongozi wa wapigania uhuru na kuanza kumsulubu kwa kipigo, huku wakimkata kiungo kimoja hadi kingine wakianzia na vidole, kiganja cha mkono na mabega ya upande mmoja na kisha upande mwingine.  Wakaja vidole vya miguu, magoti na hadi mapaja walipomaliza waliamia ya upande mwingine.


Msaidizi huyu alilia bila ya kutaja alipojificha kiongozi huyu wa wapigania uhuru-huku akifahamu yupo katika handaki kando anaposulubiwa.Cha kusikitisha damu ya msaidizi huyu ilikuwa inatiririka kwenye kigoda na kushuka hadi ndani ya handaki ambalo ndani yake alikuwamo kiongozi huyo wa wapigania uhuru.


Zoezi hilo lilifanyika hadi msaidizi huyo kukata roho na wakauwacha mwili wake eneo hilo hilo na wao kuondoka zao.


Kiongozi wa wapigania uhuru alijificha hapo kwa siku kadhaa hadi walipofika kikosi kingine cha upande wao na kuuchukua mwili wa msaidizi huyo kwa maziko ya heshima na wao kuendelea na mapigano na mwishoni kushinda vita hivyo.


Baada ya vita hivyo, kiongozi huyo wa wapigania uhuru alirudi kwao na kuwa rais taifa lao hadi hiii leo 2015, narudi kusema kuwa kiongozi huyo ni rais wa taifa mojawapo la Afrika hadi hii leo 2022.


Swali la kujiuliza ni Je damu ya msaidizi huyu wa wapigania uhuru inaweza kulipwa kwa nini?


Je DHAHABU, ALMASI, MANE MANE , LULU, FEDHA au TANZANITE?


Mwanakwetu! Nakwambia hapo si Tanzanite, Fedha, Mane mane, Lulu, Almasi wala  Dhahabu inaweza kulipa damu ya msaidizi huyo wa Kiongozi Wapigania Uhuru.


Bali cha kufanya kwa kiongozi huyo ni kuhakikisha taifa lake linawasaidia wananchi wake wanatapa maendeleo katika nyanja zote na huko kutakuwa ni kulipa damu hiyo iliyopotea ya msaidizi huyu wa Kiongozi wa Wapigania Uhuru na wapiga uhuru wote waliopoteza uhai wao kulikomboa bara letu la Afrika.

Naweka kalamu yangu chini kwa kusema kuwa harakati za ukombozi wa Afrika haikuwa singeli au lele mama ilikuwa ni kazi kubwa inayopaswa kuheshimiwa na kila mmoja wetu leo hii. Inaposemwa Machi 23 ni siku ya ukombozi wa nchini kusini mwa bara na Afrika maana yake wapo waliopigania hilo hadi kufa.


Hadi sasa siye akina mwanakwetu tumekuwa huru


Nakutakia siku njema.


makwadeladius@gmail.com

0717649257

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI