Na Amon Mtega_ ,Mbinga
KATIBU wa Chama Cha Mapinduzi CCM Wilaya Mbinga Mkoani Ruvuma Jacob Silay amewataka wanachama wa chama hicho kwenye Wilaya hiyo kuendelea kujisajili uanachama wao kwenye mfumo wa Kielektroniki ili kuendana na teknolojia ya kisasa.
Wito huo ameutoa wakati wa uzinduzi wa kadi mpya za wanachama wa CCM ambazo zimetolewa kwa mfumo wa Kielektroniki kwa baadhi ya wanachama wa kata 48 za Wilayani humo kwenye mkutano wa baraza maalumu kwaajili ya uzinduzi huo ambapo kadi 168 zilitolewa kwa wanachama hao.
Silay amesema kuwa Chama kinaendelea kufanya maboresho zaidi ya mifumo ikiwemo kumtambua mwanachama kwa mfumo wa kisasa hivyo ni vema kila mwanachama aende kwenye ofisi za CCM na kukutana na mtehama ili aweze kusajiliwa kadi yake kwa mfumo wa kisasa.
Akizungumzia sifa za mfumo wa kisasa amesema kuwa mwanachama kumbukumbu zake zote zinahifadhiwa kitalaam kwa njia ya kisasa na kuwa pindi mwanachama anapohitaji kugombea uongozi au kumchagua kiongozi taarifa zake zitatumika kuangaliwa kwa kutumia kadi hiyo.
Katika hatua nyingine katibu huyo amezitaka kila kata kuwa na simu ya kisasa ambayo itatumika kufanyia usajili ambapo baadhi ya kata tayari wameshakamilisha zoezi la kuwa na simu hizo.
Kwa upande wake mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mbinga Beda Hyera alisema kuwa kadi hizo pia zitaondoa tatizo la kuwepo kwa wanachama mamluki ambao wamekuwa wakiingia kipindi cha uchaguzi .
Hyera amesema kuwa kipindi cha nyuma kabla ya mfumo huo kulikuwa na baadhi ya watu kujifanya ni wanachama wa CCM na kuijiingiza kwenye kupiga kura na mwisho wa siku ilikuwa inaleta malalamiko kwenye chama.
Naye katibu wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya Mbinga Angelo Madundo amesema kuwa mpango wa kadi hizo utamsaidia sana mwanachama hata akiwa nje ya Wilaya yake tarifa zake zitakuwa wazi ambazo hazina mashaka.
Pia mjumbe wa kamati ya utekelezaji katika Jumuiya ya Wanawake UWT Wilaya ya Mbinga Tulizo Mtuka amesema kuwa tayari ameshapita kwenye kata mbalimbali za Wilayani humo kwa wanawake wa Jumuiya hiyo kuwahamasisha kujisajili kwa mfumo wa kisasa .
0 Comments