Header Ads Widget

WAIRAN WAZUNGUMZIA MASHAMBULIZI YA ISRAEL WASEMA HAKUNA MAHALI SALAMA

 

"Yamekwama". Hilo ndilo neno ambalo baadhi ya watu ambao wamezungumza na BBC wamekuwa wakilitumia kuelezea maisha nchini Iran hivi sasa.

Baada ya siku tatu za mashambulizi ya Israel, "kila mtu anajaribu kuitoroka" Tehran "kwa njia moja au nyingine," mkazi mmoja aliiambia BBC.

Siku ya Jumapili, foleni ndefu zilishuhudiwa katika vituo vya mafuta kote jijini. Watu walikuwa mbioni kuelekea maeneo mengine, mbali na shabaha yoyote inayowezekana kulengwa na Israeli, lakini hawakuweza hata kutoka nje ya jimbo hilo kwa sababu ya msongamano mkubwa wa magari.

"Ni wazi, Tehran sio salama," mkazi mmoja alisema. "Hatupati ving'ora au maonyo kutoka kwa maafisa kuhusu mashambulizi ya Israel. Tunasikia tu milipuko na tunatumai mahali petu hatutapigwa. Lakini tunaweza kwenda wapi? Hakuna mahali tunapohisi salama."

Mtu mmoja ambaye alifanikiwa kuhama kutoka Tehran kwenda mkoa mwingine alisema: "Sidhani nimekubali kikamilifu kwamba ninaishi katika eneo la vita, na sina uhakika ni lini nitaweza kukubali hilo."

"Hii sio vita vyangu. Sihusiki kwa njia yoyote, nataka tu kuishi pamoja na familia yangu."

Tangu Ijumaa, Israeli iliipiga Iran kwa wimbi lake kubwa zaidi la mashambulizi ya anga kuwahi kushuhudiwa kwa miaka.

Mashambulizi ya Israeli yamesababisha ulipizaji kisasi kutoka kwa Iran, ambayo imeanzisha mashambulizi ya makombora dhidi ya Israeli.

Takriban watu 10 wameuawa nchini Israeli, mamlaka ilisema. Vyombo vya habari vya Irani, vikiinukuu wizara ya afya, viliripoti kuwa watu 128 walikuwa wameuawa katika mashambulizi ya Israeli kufikia saa sita mchana Jumamosi.

Muiran mmoja aliiambia BBC kuwa hajaweza kulala kwa usiku mbili: "Nimepitia hali ngumu sana."

Alisema hali ya sasa inamkumbusha milipuko ya mabomu ya wakati wa vita vya Iran na Iraq vya miaka ya 1980, alipokuwa mtoto.

"Tofauti ni kwamba wakati huo, angalau wakati shambulio lilipotokea, tulisikia king'ora cha uvamizi wa anga au angalau maonyo kabla ya kutokea. Lakini sasa, wakati wa shambulio hili la bomu au shambulio lolote la anga, hakuna ving'ora au maonyo."

Vijana, waliozaliwa baada ya vita, hawajui ilikuwaje, Ghoncheh Habibiazad wa BBC News Persia alisema.

Mwanamke mmoja huko Tehran alisema amefikiria kuondoka jijini ili kutoroka mashambulizi hayo.

"Sote tumetaka kwenda miji midogo au vijiji, popote tunapoweza kwenda, lakini kila mmoja wetu ana wapendwa ambao hawawezi kuondoka, na tunawafikiria," alisema. "Tunachopitia sio haki kwa yeyote kati yetu, watu wa Iran."

"Sote tunajaribu kuvuka siku hizi kwa hofu, uchovu, na mafadhaiko mengi, hii ni hali ngumu sana na ya chungu."

Mkazi mmoja katika mji mkuu alisema: "Siwezi kuondoka tu Tehran. Siwezi kuwaacha wazazi wangu wazee ambao hawawezi kusafiri mbali na kwa muda mrefu na kuondoka jijini mwenyewe. Mbali na hilo, ninahitaji kufanya kazi. Nifanye nini sasa?"


Watu walipanga foleni kwenye magari mjini Tehran kupata petroli siku ya Jumapili

Mtandao haujawa thabiti, kwa hivyo ni vingumu sana kuwasiliana na watu ndani ya nchi.

Baadhi ya wale wanaoishi nje ya nchi wanatuma ujumbe kwa wapendwa wao, kuwajulia hali wakitumaini kupata jibu.

Wengine wamepokea onyo kutoka kwa jeshi la Israel wakiwatakiwa kuondoka maeneo yaliyo karibu na kabi za kijeshi. Watu huko Tehran wanaonekana kuwa na wasiwasi zaidi juu ya hili.

"Tutajuaje maeneo ya kijeshi yako wapi na wapi?" mmoja alisema. Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu katika ujumbe kwa Wairani siku ya pili ya mashambulizi hayo alisema "wakati umefika" kwa Wairani kuungana " kwa kutetea uhuru wako".

Hata hivyo, watu nchini humo mpaka sasa wameamua kusalia kimya na hakuna ushahidi unaoashiria wito wa Netanyahu umetiliwa maanani, Daryoush Karimi wa BBC News Persia alisema.

Tehran imeshuhudia mashambulizi kadhaa tangu Ijumaa


Tehran imeshuhudia mashambulizi kadhaa tangu Ijumaa

Ndani ya Iran, kile ambacho labda kiliwashtua watu zaidi ni uharibifu wa majengo ya makazi, hata zaidi ya mashambulizi ya vituo vya nyuklia na vituo vya ndege, alisema Pouyan Kalani wa BBC News Persia.

Wairani wengi hawajawahi kushuhudia matukio kama hayo tangu kumalizika kwa vita vya Iran na Iraq - hasa katika mitaa ya mji mkuu.

Baadhi ya wale walio Tehran na kwingineko, wanakumbuka taharuki ya siku ya Ijumaa, wanajiuliza : ni nini hasa kilichokuwa kikitokea; mashambulizi yalienea kiasi gani; Na wangewezaje kujilinda wenyewe na familia zao?

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI