NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
MADIWANI wa Halmashauri ya Moshi mkoani Kilimanjaro, wameiomba Serikali kutataua changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama inayowakumba wananchi kwenye kata zao.
Hayo yamejiri wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo, wakati wakichangia hoja ya taarifa ya maji ya RUWASA ya utekelezaji wa shughuli za miradi kwa Robo ya Pili kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2021.
Madiwani hao walisema kuwa kero maji hususan kwenye maeneo ya vijijini imekuwa ya muda mrefu huku wakihitaji Serikali iwasaidie kusambaza mabomba kwa wingi na kuepusha kufuata maji kwa umbali mrefu.
Akizungumza Diwani wa Kata ya Uru Kusini Wilhard Kitali, amesema kata nyingi za wilaya ya Moshi vijijini zinakabiliwa na changamoto hiyo ya upatikanaji wa Majisafi na salama, na kuwaomba RUWASA fedha ambazo wamezipata waweze kuzitumia vizuri ili kuhakikisha kwamba, huduma ya maji safi na salama inamfikia kila mwananchi kwenye eneo lake.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Mbokomu, Raphael Matemu, na Diwani wa Kata ya Marangu Magharibi Filbert Shayo wamesema kata zote 32, zilizoko katika halmashauri ya wilaya ya Moshi vijijini zinakabiliwa na changamoto ya maji na kuziomba mamlaka zinazohusika na maji kuhakikisha kwamba wanatatua changamoto hizo ili wananchi wa maeneo hayo waweze kupata maji kwa uhakika.
Awali akisoma taarifa hiyo kwa niaba ya Meneja wa Ruwasa Moshi Vijijini Mtaalamu wa Maji Juu ya Ardhi Alice Irira, amesema kuwa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kwa mwaka wa fedha 2021/2022, imetengewa fedha kiasi cha shilingi bilioni 3.13 ikiwa ni fedha za Mfuko wa maji na fedha za UVICO-19 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya majai wilayani humo.
Aidha Mtaalamu huyo amesema RUWASA imejipanga kuhakikisha kwamba miradi yote ya maji ambayo wananchi walikuwa wakitumia maji bila kuwa na mita, uongozi wa RUWASA wilaya ya Moshi, wanajipanga kwenda kuwafungia wananchi mita za maji ili waweze kupata maji kwa uhakika na kuweza kulipia gharama hizo za maji.
MWISHO.
0 Comments