Na. Andrew Chale,
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Kassim Majaliwa anatarajiwa kumwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika kilele cha sherehe za miaka 50 ya Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Juni 17, 2025 makao makuu ya Taasisi hiyo, Bagamaga Dar es salaam.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dkt. Aneth Komba wakati wa Semina kwa Wahariri na Waandishi wa Habari kuelekea miaka 50 ya Taasisi hiyo, iliyofanyika leo Juni 13, 2025 Makao makuu ya Bamaga.
![]() |
Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dkt. Aneth Komba |
Katika semina hiyo Viongozi wa TET wamepata kuwasilisha taarifa mbali mbali kwa kina ikiwemo mafanikio na namna ilivyofanikiwa kukuza elimu nchini kupitia majukumu yake.
Aidha, viongozi wameelezea matarajio ya TET katika kuadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1975 na kuwaomba wahariri na waandishi wa habari kuendelea kuwaunga mkono katika kutangaza kazi mbalimbali za TET.
Awali akiwasilisha taarifa katika semina hiyo, Dkt. Aneth Komba amebainisha kuwa katika kipindi cha miaka 50 wameweza kuandaa kamusi ya kwanza ya lugha ya alama ya Tanzania.
Dkt. Komba amesema kamusi hiyo ya ufundishaji na ujifunzaji wa wanafunzi viziwi kuanzia elimu ya awali mpaka vyuo vikuu mbalimbali hapa nchini.
“Kamusi hii imepakiwa katika vishikwambi walivyopewa wanafunzi husika na inapatikana pia katika tovuti www.tie.go.tz,” amesema na kuongeza:
Wamefanikiwa kuandaa vitabu vyote vya kiada pamoja na kiongozi cha mwalimu kuanzia ngazi ya elimu ya awali mpaka ualimu kwa shule zinazotumia Kiswahili na Kiingereza kama lugha za kufundishia.
“Pia tumefanikiwa kutafsiri vitabu vyote vya kiada katika maandishi ya breli na yaliyokuzwa kwa matumizi ya wanafunzi wasioona na wenye uoni hafifu mtawalia.
“Ndani ya miaka 50 ya TET imefanikiwa pia kuchapa na kusambaza vitabu vya kiada vya kimacho kwa masomo ya sayansi kwa uwiano1:1. Kuchapa na kusambaza vitabu vya kiada vya masomo mengineyo kwa uwiano wa 1:3,” amesema Dk. Komba.
0 Comments