TAZAMA FULL VIDEO YA MAZISHI BOFYA HAPA
NA MATUKIO DAIMA MEDIA
Mbunge wa Jimbo la Ismani ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mheshimiwa William Lukuvi, ametoa shukrani za dhati kwa wapiga kura wake kutoka vijiji vyote vya Jimbo la Ismani kwa kujitokeza kwa wingi katika msiba wa mdogo wake, Xavier George Lukuvi.
Akizungumza Jumamosi katika mazishi yaliyofanyika Idodi, mkoani Iringa, Mheshimiwa Lukuvi alisema kuwa kitendo cha wapiga kura wake kuungana naye katika kipindi hiki kigumu ni ishara ya mshikamano, upendo na mshikamano wa kweli kati ya viongozi na wananchi wao.
Katika hotuba yake fupi ya shukrani, Lukuvi alisema kuwa aliguswa sana na moyo wa kujitolea wa wananchi waliokodi magari kwa gharama zao kwenda Idodi, umbali wa kadri, ili kutoa pole na kumfariji kwa majonzi aliyoyapata kutokana na kifo cha mdogo wake.
Alisema kuwa anaamini kuwa upendo huu wa kweli ni matokeo ya mahusiano mazuri na ya karibu aliyoendeleza na wananchi wake kwa kipindi chote akiwa mbunge wa Ismani.
Mbali na wananchi, Lukuvi pia aliwashukuru viongozi wa chama na serikali walioungana naye katika msiba huo mzito.
Alisema uwepo wao haukuwa tu faraja kwake binafsi na familia ya marehemu, bali pia ni uthibitisho wa mshikamano wa kitaifa unaoonyeshwa wakati wa huzuni.
Viongozi waliokuwa miongoni mwa waliomhurumia na kumfariji Lukuvi ni pamoja na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Salim Abri Asas aliyemwakilisha Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mshauri wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan – Rajab Lwuhavi, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Peter Serukamba, pamoja na wakuu wa wilaya, wabunge na viongozi wengine wa serikali na chama waliowasili kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.
WASIFU WA MAREHEMU XAVIER GEORGE LUKUVI
Xavier George Lukuvi alizaliwa tarehe 4 Machi, 1969 huko Mapogoro, Idodi mkoani Iringa.
Alianza elimu ya msingi mwaka 1979 katika Shule ya Msingi Kitanewa, na baadaye alihitimu elimu hiyo mwaka 1985 katika Shule ya Msingi Isupilo.
Mwaka 1986 alijiunga na Shule ya Sekondari Ifunda na kuhitimu kidato cha nne mwaka 1989.
Baada ya sekondari, mwaka 1990 alijiunga na Chuo cha Ufundi Arusha kwa ajili ya masomo ya Astashahada (Full Technician Certificate) katika fani ya uhandisi wa majengo na kuhitimu mwaka 1993.
Aliendelea kupanua maarifa yake ya kitaaluma mwaka 1999 alipojiunga na Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) ambapo alitunukiwa Stashahada ya Juu katika Teknolojia ya Habari (Advanced Diploma in Information Technology) mwaka 2002.
Aliendelea na masomo ya juu zaidi nchini India ambapo mwaka 2007 alihitimu Shahada ya Uzamili ya Tehama (Masters Degree of Computer Applications) kutoka Chuo Kikuu cha Hyderabad na shahada nyingine ya Uzamili ya Usimamizi wa Biashara (MBA in Information Technology) kutoka Chuo Kikuu cha Sikkim.
UTUMISHI KAZINI
Xavier alianza ajira rasmi tarehe 17 Oktoba 1995 katika Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), wakati huo ukiitwa Shirika la Akiba ya Taifa ya Wafanyakazi (NPF).
Alianza kazi kama Kalani wa Majengo (Estate Clerk) katika Makao Makuu ya NSSF. Kwa kipindi cha miaka 30 ya utumishi wake, alifanya kazi kwa weledi mkubwa akichangia mafanikio ya miradi mbalimbali ya kimkakati ya shirika hilo.
Kati ya nafasi alizowahi kushikilia ni Meneja wa Mkoa wa NSSF Temeke kuanzia Novemba 2018 hadi Februari 2020 ambapo alihamishiwa Shirika la Taifa la Madini (STAMICO).
Kabla ya kifo chake, alikuwa Afisa Matekelezo Mkuu wa NSSF Mkoa wa Morogoro.
Alijipambanua kwa kuwa mtendaji makini, mchapakazi, na mwenye mchango mkubwa katika maendeleo ya taasisi alizozitumikia.
UGONJWA NA KIFO
Mwaka 2024, Xavier alianza kuumwa na aligundulika kuwa na saratani ya utumbo. Madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili walimshauri apelekwe India kwa matibabu zaidi.
Kwa msaada wa Serikali kupitia waajiri wake NSSF na NHIF, alipelekwa katika Hospitali ya Appolo, New Delhi tarehe 25 Septemba 2024, ambako alikaa kwa matibabu hadi Machi 2025 aliporejea akiwa na nafuu.
Hata hivyo, hali yake ilianza kuzorota tena Mei 2025. Alitarajiwa kurudi India kwa vipimo zaidi, lakini hali ilibadilika ghafla tarehe 28 Mei na akalazwa tena Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Usiku wa kuamkia tarehe 2 Juni 2025, hali yake ilizidi kuwa mbaya na kupelekwa ICU. Licha ya jitihada za madaktari, alifariki dunia saa saba mchana kutokana na kushindwa kwa moyo wake kuendelea kufanya kazi.
MAISHA YA FAMILIA NA IMANI
Marehemu Xavier ameacha mjane, Bi. Lidya Mark Leo, na watoto watano wote wa kiume: Collins, Victor, Vallen, Vinn, na Vian Xavier Lukuvi.
Alikuwa Mkristo Mkatoliki wa imani thabiti aliyepewa Sakramenti za Kanisa: Ubatizo, Kipaimara na Ndoa Takatifu.
UANACHAMA NA SHUGHULI ZA JAMII
Xavier alikuwa mwanachama mwaminifu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na mfuasi wa kweli wa klabu ya Simba SC.
Alifuatilia kwa karibu michezo ya klabu hiyo, na hata akiwa amelazwa hospitalini aliomba kuangalia mechi muhimu kati ya Simba na Singida Black Stars, licha ya kuwa matokeo hayakuwa ya kuridhisha.
MAFUNZO KUTOKA MAISHANI MWAKE
Marehemu ameacha alama kubwa ya upendo, mshikamano, uadilifu, uchapakazi, na moyo wa kusaidia wengine.
Aliheshimika kama mshauri mzuri, mwenye uvumilivu, mzalendo, na rafiki wa kila mtu bila kujali hadhi wala uwezo wa mtu. Alikuwa tegemeo kwa wengi waliomzunguka.
SHUKRANI
Familia ya marehemu imetoa shukrani za dhati kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa msaada wa kimatibabu.
Pia wanashukuru madaktari na wauguzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili na Hospitali ya Appolo India kwa huduma bora, pamoja na ndugu, jamaa na marafiki wote waliotoa msaada wa hali na mali.
Kwa hakika, kifo cha Xavier George Lukuvi kimeacha pengo kubwa, lakini pia kimeacha urithi wa maadili, kujituma, upendo na mshikamano wa familia na jamii.
Bwana alitoa, Bwana ametwaa, jina la Bwana lihimidiwe.
0 Comments