Header Ads Widget

KISARAWE KWENDA KIBAHA ( II )

 



Adeladius Makwega_Dodoma.


Baada ya safari ndefu kutoka Tazara, Buguruni, Ubungo Maji, Vigwaza na sasa tulikuwa katika kijiji cha Kimara Misale wilayani Kisarawe huku  tukikaribishwa na vilio vya wadudu kutambulisha kuwa sasa tupo kijijini.


Kiliandaliwa chakula kikaweka katika msala na kukaribishwa, nilishangaa chakula hicho kilikuwa kingi mno lakini tuliambiwa kuwa chakula hicho ni chenu basi tulianza kula ulikuwa ni wali na nyama ya kuku. Wakati tunakula nilibaini kuwa havikuungwa na nazi wala mafuta.


Mwanakwetu nilikuwa chakula hicho vizuri sana ambacho kilikuwa kitamu mno na kwa hakika hadi mwisho tulimaliza sinia lote la wali na nyama hizo za kuku.


Nakumbuka utamu wa chakula hicho sijawahi tena kuupata tangu wakati huo hadi leo mapishi ya bibi huyo ambaye alikuwa na miaka kama 68 wakati huo yalinishangaza mno. Kwanza nilistaajabu kula chakula kingi, utamu wake na kikiwa hakina viungo zaidi ya chumvi na kitunguu tu.


Nilitafakari mapishi hayo, nilibaini kweli kupika ni sayansi nyengine, nilimpenda aliyepika chakula hicho na kwa kuwa nilikuwa kijana ambaye nilikuwa sijaoa nilitamani kuwa na mke anayetambua kupika kama bibi huyo. Nikasema kweli mume wa bibi huyu anafaidi mno mapishi hayo. Nilisema moyoni kama mapisho hayo mambo ni moto,je vipi katika mapishi yale mengine? Lakini nikasema bibi huyu ameshastaafu yale mambo mengine lakini nikasema hata Michel Platin umahiri wake wa soka unapaswa kusifiwa kwa sasa.


Mara baada ya kula nilizungumza na ndugu hawa ambapo walikuwa ni watu wazima sana, mzee wa familia hii alikuwa akifahamika kama Seleimani Zoka Bin Mangala na mkewe Habiba Mwinshehe Sami Binti Mangala. Ndugu hawa walikuwa makabila mchanganyiko kuna Uzaramo, Ukwere, Uluguru na Upogoro ndani yao.

Nililala salama katika kitanda cha kamba na mkeka na asubuhi niliwasiliana na Mtangazaji Chunga Ruza na kutuma ripoti ya asubuhi redioni kwa hakika Kimara Misale mitandao ya simu ilikuwa haipatikania kwa hiyo kuwasiliana na Chunga Ruza ilibidi kupelekwa kwenye kichuguu ndipo tulipopata mtandao wa simu. 


Nilipoamka nilibaini kuwa Bibi Habiba Binti Magala ambaye ukoo wake unafanana na wa mumewe kuwa hawakuwa ndugu bali koo zao zinafanana majina tu. Binti Mangala huyu ambaye alikuwa bibi mmoja mrembo, mnyenyekevu, anajua kupika na mkarimu kwa wangeni.


Asubuhi hii niliukumbuka wali ule wa nyama ya kuku isiyoungwa ulivyokuwa mtamu. Nilimfananisha bibi huyu na warembe kadhaa ambao niliwahi kuwaona kwa macho yangu labda urembo wa Bibi Habiba ulikuwa ukilingana dada yangu Mbiki Msumi ambaye alikuwa ni Miss Tanzania nambari mbili mwaka 2002.


Habiba Binti Mangala nilizunguma naye kwa kirefu sana ambaye japokuwa alikuwa mtu mzima aliniamba habari nyingi za Dar es Salaam wakati akiwa mwanamwali na mumewe ambazo msomaji wangu nitakusimulia katika matini zijazo, tulikunywa chai na kuelekea katika mkutano huo wa mgogoro baina ya wakulima na wafugaji.


Kikao kilitanguliwa na vikao vya ndani ambao ofisi ya Wilaya ya Kisarawe ilimtuma Afisa Ardhi na Mkuu wa Polisi wa Wilaya(OCD). Pale kijijini walikuwapo mwenyekiti wa kijiji na wajumbe wake. Nilibaini kuwa OCD Kisarawe alikuja amekamilipa hata kungetokea lolote angeweza kutuliza ghasia.


Viongozi wa kijiji wakituhumiwa kuwauzia wafugaji ardhi huku na wao wakijibu kuwa hoja hizo hazikuwa za kweli. Kijiji hiki kilikuwa hakina mtendaji wa kijiji, kazi za mtendaji alikaimishwa mwalimu wa shule ya msingi ambaye ndiye alikuwa mwandishi wao.Mwalimu huyu alikuwa na mwandiko mzuri sana, alikuwa akiumba herufu kama anachora vile ndiye alikuwa mkuu wa shule ya msingi.


Kabla ya kikao hicho niliongea naye na alinisimulia namna maisha yake ya kazi yalivyo magumu na changamoto za siasa za kijiji hicho huku akisema kuwa mwaka 2012 akienda masomoni.


Kikao kilifanyika na mgogoro huo kutatuliwa vizuri mno. Huku wananchi hao wakimkumbuka Kapteni Lyamungu namna alivyojenga daraja lao ambalo lilibomoka kwa mafuriko. Huku akiwa Mkuu wa Wilaya rafiki wa watu wa Kimara Misale.


Maswali ya mgogoro huo yalipokwisha mada iliangukia kwenye maswali ya mambo mengine ya kijiji hicho ikiwamo uhaba wa watumishi katika zahanati yao, uhaba wa walimu na mambo mangine mengi.


Je maswali hayo ya uhaba wa watumishi wa afya, uhaba wa wlaimu, kubomoka kwa daraja yanaweza kujibiwa na Afisa Ardhi wa wilaya na OCD? 


Kwa hekima walisema kuwa leo tumekuja kutatua mgogoro wa ardhi tu haya mengine tunayapeleka kwa wakubwa Kisarawe na tutawapa majibu yake.Kikao kilikamilika na sote kurudi makwetu.


Kwa hakika hayo ni mambo ya miaka 11 iliyopita na Februari 10, 2022 niliumwa sikio kuwa kijiji cha Kimara Misale sasa kimehamishiwa Wilaya ya Kibaha na hakipo tena Kisarawe, huku mara baada ya kuhamshiwa wilaya nyingine barabara yao inajengwa na hata lile Daraja la Kapteni Lyamungu lililobomoka sasa limejengwa. Wanadai kuwa wamejengewa shule nzuri sana na ina walimu wa kutosha, zahanati yao ina wahudumu wa kutosha, wamewekewa mabomba ya maji safi. Hata zile safari ndefu za kuvuka mto na kwenda Wilayani Kisarawe hazipo bali wanakwenda Kibaha.


Nina imani Mungu akinijalia nitakwenda kumtembela Bi Habiba binti Mangala na mumewe huko Kimara Misale ili nikaule ule wali na nyama ya kuku asiyeungwa na nijue hali ya maendeleo ya kijiji hicho kwa macho yangu.


Mwanakwetu kwa leo naishia hapo kwa hii safari ya kijiji cha Kimara Misale kutoka Wilayani Kisarawe na kuhamishiwa Kibaha.


Nakutakia siku njema.


makwadeladaius@gmail.com

0717649257

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI