Header Ads Widget

KISARAWE KWENDA KIBAHA ( I )

 



Adeladius Makwega_ Dodoma.


Nilijulishwa na ndugu yangu Hassani Mbazigwa kuwa kuna safari ya kwenda Kijiji cha Kimara Misale Wilaya ya Kisarawe mkoa wa Pwani wakati huo, kwani huko kuna mgogoro baina ya wakulima na wafugaji.


Mbazigwa alinijulisha kuwa safari hiyo nitakwenda na bwana mmoja ambaye huko ni kwao na alikuwa maarufu sana kwani alikuwa na urafiki mwingi na watangazaji wengi wakongwe wa shirika nililokuwa nafanyia kazi.


Nilipojulishwa hilo nilirudi nyumbani kwetu Mbagala, kwa kuwa nilikuwa bado kijana sikuwa na familia, niliporudi nyumbani nilimjulisha bibi yangu mzaa Baba Edwiki Omary Binti Mkomangi kuwa kesho ninaenda safari, kwa hiyo kwangu sintokuwepo mmojawapo wa jamaa zangu aende kulala kulinda makazi yangu.


Kweli kulipokucha nilielekea kazini nikiwa na begi langu la vifaa vyangu vya kazi, nlipofika kazini nilifanya kazi kwa haraka haraka na saa saba ilipofika nilipigiwa simu na ndugu huyo aliyekuwa na mfanyabiashara wa soko la Buguruni kuwa sasa tunatakiwa kuanza safari ya kwenda huko Kimara Misale kwenye kikao cha kutatua mgogoro huo ambapo kilitakiwa kufanyika kesho yake.


Nilitoka Tazara hadi Buguruni, tukapanda daladala hadi ubungo, tuliposhuka ubungo tukatembea kidogo hadi Ubungo Maji, hapa tukapanda basi linaloelekea Chalinze. Tulipanda basi ambalo lilikuwa limejaa mno lakini kwa bahati njema mimi na mwenyeji wangu huko tuendako tulipata siti.


Safari iliendelea hadi tunafika Vigwaza, ilikuwa kama saa 10.30 jioni, tukashuka vizuri na kuutafuta usafiri wa bodaboda ambao kwa wakati huo bodaboda walikuwa wachache sana na vijana walikuwa na bodaboda walikuwa wazaliwa wa Kimara Misale. Tuliwagonja hapo kwa nusu saa walirudi kwa sababu yetu kwani abiria kwa mida ya jioni huwa wachache mno. 

Tulipata bodaboda mbili, mimi nilipanda ya kwangu na mwenyeji wangu alipanda bodaboda yake.


Mwanakwetu kuna umuhimu mkubwa wa kila abiria kupanda bodaboda yake kwanza hata kama inatokea ajari kidogo madhara yanakuwa kiasi lakini pia siyo ustaarabu watu wazima kubahashiana katika bodaboda moja.


Nikiwa katika bodaboda hii nilijifunza mambo makubwa matatu, kwanza maana ya jina Kimara Misale kuwa ni eneo hilo lilikuwa na wanyama wengi, kwa hiyo wawindaji wa Kizaramo, Wakwere, Waruguru,Wakaguru na hata Wapogoro walikuwa wakiwinda ili kuweza kuishi kwa raha na kula nyama ujanja wa wakati huo ulikuwa ni kuwa na mishale tu. Maana ilisadia mno katika uwindaji, kwa hiyo eneo hilo hadi sasa ni Kimara+Misale. Kwahiyo Kimara ni jina Kimara na Misale ni Mishale.


Jambo la pili nililojifunza lilikuwa ni umbali kutoka Vigwaza hadi Kimara Misale kwa miguu ulikuwa ni mwendo wa siku nzima na kwa bodaboda ni mwendo wa saa tatu hadi nne. Kwa hakika ujio wa bodaboda umesaidia mno kuyafanya maisha kuwa mepesi.


“Zamani mtu akiwa na pikipiki ni bwana shamba au bwana mifugo wa kijiji na hizo zilikuwa ni zile 110 au XL tu. ”Aliniambiwa mwenyeji wangu tuliyekuwa tunaenda naye KImara Misale.


La tatu japokuwa Kimara Misale ilikuwa Wilaya ya Kisarawe, kutokea Tazara Kisarawe kwa kupitia Barabara ya Pugu (sasa Nyerere) ni jirani mno, lakini ni heri kuzunguka Vigwaza kwani kijiji hicho kilikuwa jirani na Wilaya ya Kibaha Vijijini kulikoni Wilaya ya Kisarawe.


Mwanakwetu safari hiyo iliendelea huku tukipita katika mabawe (mashamba ya mpunga) kwa desturi mabawe ya mpunga wakati wa mvua hujaa maji mengi na hapo ndipo mpunga hupandwa.


Udongo wake ulikuwa mweusi ambao ulikuwa umekatika katika na njia hii ilikuwa ikipita sana baiskeli na magari machache ya kubeba mikaa na magari ya mazao msimu wa mavuno.


Tukiwa safari tulikutana na daraja moja kubwa ambalo lilibomoka vibaya ambalo vijana hawa bodaboda walisema kuwa lilikatika msimu wa mvua wa mwaka 2010. Sasa ili kupita tuliingia chini ya daraja lililobomoka nikiambiwa kuwa mvua zikinyesha hapapitiki kabisa kwa kuwa eneo hilo mto Ruvu unapita.


Vijana hawa walinisimulia kuwa daraja hilo lilijengwa zamani sana enzi za Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Kapteni Mstaafu James Lyamungu ambaye alifika eneo hilo na kuelezwa shida yao ya daraja ndipo alipofika na taasisi ya Ujenzi wa Barabara ya wakati huo Tanzania Road Maintenance (TRM) na wakalijenga.


“Kapteni Lyamungu alikuwa mwanajeshi, alisimamia ujenzi wa daraja hilo tangu mwanzo hadi mwisho lakini sasa limebomoka. Alikuwa akija kijijini kwetu na tulifanya naye shughuli za maendeleo kila mara, japokuwa sisi tulikuwa mbali mno na Kisarawe, ofisini kwake.” Waliniambia vijana hawa wa bodaboda.


Kwa kuwa safari ilikuwa ndefu niliwauliza pia juu ya Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe wakati huo walinijibu kuwa hawamfahamu, bali walikuwa wakimfahamu mbuge wao za zamani Athumani Janguo na mbuge wao mpya Selemani Jafo.


Niliwauliza juu ya habari za Kapteni James Lyamungu waliniambia kuwa kuwa mwaka huo 2011 alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Serengeti.


“Kapteni Lyamungu tunamfuatilia bado anachapa kazi hadi sasa, yule alikuwa mkuu wa wilaya rafiki wa watu wa Kisarawe.” Alisema mwenyeji wangu huku akiwa amepakiwa katika bodaboda ya mbele.


Basi ilipofika saa moja kamili. tulifika katika kijiji cha Kimara Misale na kupokelewa na wenyeji wangu hawa.


Je itakuwaje katika safari hiyo subiri makala ijayo. Nakutakia siku njema.

makwadeladaius@gmail.com

0717649257

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI