Header Ads Widget

MKUBWA TAZAMA

 




Siku ya leo nilimpigia simu ndugu yangu anayefahamika kama Idi Langweni, mkaazi wa Kijiji cha Mwanadilatu huko Mkuranga Pwani. Kuulizia hali ya hewa, ndugu yangu huyu aliniambia kuwa huko kwetu mvua imenyesha vizuri sana, tangu Novemba 31, 2021 hadi Disemba 31, 2021 ila tangu Januari 1 -6, 2022 mvua imepumzika kidogo. Nilijulishwa kuwa waliopanda kunde, mpunga, mihogo na mazao mengine wamefanya hivyo, akisema kuwa Mkuranga njaa mwaka huu hakuna..........Adeladius Makwega_Dodoma.



Nilimtania ndugu yangu Langweni kuwa au siku hizi mnatambika Pwani na Bara? Mnafunga safari kwa ndugu yenu Hussein Mwinyi, mnatambika, alafu mkirudi tena Mkuranga mnatambika, ndiyo maana mnapata neema hiyo ya mvua? Iddi Langweni alicheka tu, hakusema ndiyo au hapana.


Hali hii ya mvua imekuwa tofauti na Chamwino kwani kwa kumbukumbu zangu eneo la Chamwino Ikulu kama mvua imenyesha kwa kipindi hicho ni mara moja tu yaani usiku wa mwaka mpya Disemba 31, 2021.


Kwa hesabu za namba, Chamwino Ikulu wana siku moja ya mvua, wakati ndugu zangu wa Mkuranga wana mtaji wa siku 30. Hapo kama kunde zimeota na hata unaweza kuchuma majani yake na kuyapika kama mboga kwani yana ngazi hata nne. Wakati Chamwino Ikulu, mwanakwetu mahindi yamepandwa lakini hayajaota hadi sasa.


Mazungumzo yangu na ndugu yangu huyu yalinipa nafasi ya kutafakari habari za Mkuranga za miaka 30 iliyopita inayolingana fika na neema ya hizo ya mvua zilizonyesha.


Nakumbuka kuwa mwaka 1995 hadi mwaka 2000 Mkuranga iliongozwa na Mbunge aliyekuwa akifahamika kama Mwalimu Mwinyishehe Shabani Mlao ambaye alikuwa akisomesha huko Buyuni-Pazuo na akiwashinda wagombea wengine katika uchaguzi huo wa kwanza wa vyama vingi, akiwamo ndugu yangu Adam Kighoma Malima. Wakati huo Adam ambaye sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga alikuwa mwanachama wa NRA (National Reconstraction Alliance) hiki ni chama kilichoanzishwa na Baba yake marehemu Profesa Kighoma Malima.

Katika matokeo hayo, mgombea aliyechukua nafasi ya tatu ni marehemu Zaharani Mbaruku Timo aliyekuwa mgombea wa CUF (Civic United Front) chama cha wananchi.


Wapiga kura wengi nakumbuka walivutiwa sana na mikutano ya Adam Malima hasa hasa; mosi, alivyokuwa akiongea kama marehemu baba yake, pili alikuwa mchangamfu sana jukwani kama walivyo Wazaramo, Wandengereko na makabalia mengine ya ukanda huu wa Pwani. Japokuwa Adam Malima alishindwa lakini wakaazi wengi wa Mkuranga walimpenda ndugu yao huyo namna alivyokuwa akiomba kura na hilo liliibua hoja katika vijiwe vya kahawa.


“Shinda ya huyu mtoto ya Profesa Malima ni chama chake tu, lakini ni mwanasiasa mzuri sana.” Yalitamkwa hadharani maneno hayo.


Kisiasa hakukuwa na namna ya kumuacha Adam Malima kubaki upinzani na mwaka 2005 ndipo Adam Malima alipogombea kupitia CCM na kushinda na kuwa mbunge wa Mkuranga hadi mwaka 2015 huku akishika nyadhifa za unaibu Waziri wa Mipango na Fedha .


Nilipokuwa naongea na ndugu yangu Langweni leo nilimtania juu ya matambiko yao wanayokwenda kufanya Zanzibar kwa ndugu yao Dkt. Hussein Mwinyi ambapo kwa hakika ndugu huyu siasa alizianzia Mkuranga kwa kumshinda Mwalimu Mwinyishehe Shabani Mlao katika kura za maoni za CCM(Chama cha Mapinduzi) hata katika uchaguzi mkuu Dkt Hussein Mwinyi aliaminiwa kwa kitu kimoja tu, Imani ya watu wa Mkuranga kwa Rais wa Awamu ya Pili Ali Hassani Mwinyi(Mzee Ruksa)


“Hussein atakuwa kama baba yake, tumpe kura jamani.” Alisema mzee mmoja wa Kijiji cha Mwanadilatu, Marehemu Mau kuwashawishi Wazaramo, Wandegereko na Wamakonde wa Mkuranga kumpigia kura Dkt. Hussein Mwinyi.


Wakati wa kuomba kura majukwaani Dkt. Hussein Mwinyi hakuwa mzungumzaji mzuri sana kama alivyokuwa Adam Malima mwaka 1995 na NRA, nakumbuka Adam alilimiki jukwaa vizuri sana huku akijinasibu mbele ya wapiga kura kwa mavazi yake na kusoma kwake ughaibuni . Mwaka 2000, sikumbuki Adam Malima alikwenda wapi na NRA yake lakini CUF chama cha wananchi kama nilivyokwmabia awali kuwa walimsimamisha jamaa mmoja alikuwa mrefu, mweupe sana kama mwarabu, marehemu Zaharani Mbaruku Timo, ambapo fitna mojawapo aliyopigwa ndugu Timo ilikuwa ni Uarabu wake wa kuchovya. Nakumbuka mwisho wa siku Dkt Hussein Mwinyi alishinda kwa silaha moja tu ya Imani ya wapiga kura kwa baba wa mgombea.


Sifahamu kama Dkt Hussein Mwinyi ambaye sasa ni Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi analikumbuka hili. Lakini naona Zanzibar kazi zinaenda vizuri huko na juzi amemtengea Mkurugenzi wa ZBC Dkt Salehe Yussufu Mnemo katika barua iliyosainiwa na Injinia Zena Said dada yangu mwenyewe huyu.


Ngoja nimuume sikio Dkt Hussein Mwinyi kuwa


“Tangu umtengue Dkt Mnemo kwetu Mkuranga mvua hainyeshi.”


Kwa heshima na taadhimu namuomba Dkt Hussein Mwinyi ampatie tahafifu kidogo Dkt Mneno. Lakini pia yoyote anayekosea, muite na zungumza naye, haya mambo ya kutenga na kutengua, mazito sana na yanatisha, heri uwe unatenga tu. Kwa maana tunataka mvua zinyeshe huku kwetu Mkuranga. 


Naweka kalamu yangu chini kwa siku ya leo kwa kusema kuwa Mkuranga inatokana na maneno mawili ya kibantu MKUU+LANGA, Mkuu maana yake mkubwa na langa maana yake tazama.Tatizo la kuwepo R badala ya L ni athari ya Wazaramo na Wandengerko katika herufi hizo.


“MKUBWA TAZAMA.”


makwadeladius@gmail.com

0717649257

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI