Header Ads Widget

MGOMBEA URAIS CHAMA CHA MAKINI AAHIDI EKARI 5 KWA KILA KIJANA KAMA ATASHINDA


Na Hamida Ramadhan, MatumioDaima Media Dodoma

MGOABEA urais kupitia Chama Cha Makini, Coaster  Kibonde, amechukua fomu ya kugombea nafasi hiyo katika ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), huku akiahidi iwapo watanzania watamchagua kila kijana wa Kitanzania mwenye umri wa kuanzia miaka 21 atapewa ekari  tano za ardhi kwa ajili ya shughuli za kilimo.

Kibonde anakuwa mgombea wa nne kuchukua fomu akitanguliwa na Rais Samia Suluhu Hassan na Dkt Emmanuel Nchimbi (CCM)  Kunje Ngombare Mwiru na Chumu Abdallah Juma ,Chama cha Wakulima (AAFP) na Hassan Almas na Ally Hassan (NRA).

Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu, Kibonde ambaye aliambatana na mgombea mwenza wake,  Azza Haji Suleiman, alisema kuwa serikali yake inalenga kuwahamasisha vijana kuingia kwenye kilimo cha kisasa chenye tija, badala ya kutegemea kilimo cha jadi ambacho alisema hakina manufaa ya kudumu.


“Tutafanya kilimo cha umwagiliaji ili kuachana kabisa na kilimo cha kutegemea mvua ambacho ni kilimo cha umasikini. Maana ya Chama Makini ni Maarifa, Kilimo na Nishati,” alisema Kibonde.

Aidha, alieleza kuwa wamekabidhiwa fomu 40 na sasa wanaanza mchakato wa kutafuta wadhamini katika mikoa 10 ya Tanzania Bara na mikoa 2 ya Visiwani, huku akitoa wito kwa wananchi kuwapokea kwa moyo wa uzalendo.

Elimu, Kilimo na Afya – Vipaumbele vya Chama Makini

Kibonde alisisitiza kuwa elimu itakuwa kipaumbele cha kwanza katika utawala wake huku akiweka  mkazo mkubwa katika kuhakikisha kila kijana wa Kitanzania anapata elimu ya kiwango cha kimataifa.

 “Ukimnyima Mtanzania elimu ni sawa na kumfunga gerezani maisha. Sisi tutalivalia njuga suala la elimu tutahakikisha elimu inayopatikana duniani kote inamfikia kijana wa Kitanzania,” aliongeza.


Kwa upande wa afya, Kibonde alisema serikali yake itaweka mkazo mkubwa katika kuimarisha huduma za afya nchini kwa kujenga hospitali katika kila kata pamoja na kuyapatia vifaa tiba vya kisasa.

“Ukimnyima Mtanzania afya ni sawa na kumhukumu kifo tutahakikisha tunakuwa na wataalamu wa kutosha kwa sababu tutawekeza sana katika elimu ya afya,” alisema.

Alitangaza pia kuwa serikali yake itaanzisha bima ya afya kwa wote itakayojulikana kama MakiniCare, ambayo italenga kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za afya bila ubaguzi.

Kibonde alimalizia kwa kuipongeza Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kwa jinsi ilivyoshirikisha wadau wote tangu mwanzo wa mchakato wa uchaguzi, akisema amefurahishwa na mapokezi mazuri aliyoyapata ofisini hapo.

Vyama vingine vinavyotarajiwa kuchukua fomu leo ni National League (NLD) na United People Democratic  (UPDP).


 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI