Na COSTANTINE MATHIAS, Simiyu.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Simiyu kimetangaza majina ya wagombea wa nafasi za Udiwani watakaopeperusha bendera katika Uchaguzi Mkuu 2025, ambao wamepitishwa na CCM.
Aidha Chama hicho kimewaondoa Wagombea wanne ambao waliongoza katika kura za maoni kwa kufanya mabadiliko na kuweka wengine kutokana na kukosa sifa, vigezo na mahitaji ya wananchi.
Akitoa taarifa mbele ya Waandishi wa Habari, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Mkoa wa Simiyu, Lumeni Mathias amesema kuwa Kikao Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa huo ambayo iliketi August 13, 2025 na kupitisha majina ya wagombea Udiwani katika kata 133 za Mkoa huo.
"Mkoa wa Simiyu una kata 133, Madiwani waliobahatika kuendelea na nafasi zao ni 88 na wapya ni 45 ambao wataendeleza gurudumu la kuwatumikia wananchi" amesema na kuongeza.
"Kwenye wilaya ya Bariadi yenye kata 31 (Madiwani wapya 19, wa zamani 12), Meatu yenye kata 29 (wapya 9, wa zamani 20), Maswa yenye kata 36 (wapya 10, wa zamani 26), Busega yenye kata 15 (wapya 2, wa zamani 13) na Itilima yenye kata 22 (wapya 5, wa zamani 17)".
Ameongeza kuwa mchakato ndani ya CCM umemalizika huku akiwaomba Wana CCM na wanachama kuwaunga mkono walioteuliwa na CCM kupeperusha bendera katika Uchaguzi Mkuu utaoafanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
Amewataka Wana CCM kuvunja makundi na kuunga Mkono kundi moja la Chama Cha Mapinduzi ili kushiriki Uchaguzi Mkuu wakiwa na kundi moja ambalo ni CCM.
Amesema CCM ngazi ya Mkoa wa Simiyu, imeteua Wagombea Udiwani wenye sifa na wanaokubalika kwa wananchi, ambao watakwenda kuipigania CCM kwa wananchi katika nafasi za Udiwani.
Katika hatua nyingine, Lumeni amesema kuwa wapo baadhi ya Wana CCM waliongoza kura za maoni, lakini CCM ilikuwa inaangilia vigezo ikiwemo kukubalika kwa wananchi ambapo kati ya kata 133, kata nne (4) zimefanyiwa mabadiliko.
"Vigezo hivi vimezingatia mahitaji ya wananchi ikiwemo kukubalika, kata hizo ni Sapiwi, Gibishi, Mwamtani na Mwakisandu" amesema.
Mwisho.
0 Comments