Maelefu ya watu wakiandamana alhamisi ya wiki iliyopita mjini Khartoum kuonyesha mshikamano wao na serikali ya mpito ya Sudan
Watu wenye silaha wamewakamata baadhi ya maafisa wa serikali ya mpito ya Sudan majumbani kwao, taarifa zinasema, wakati huu mzozo wa kisiasa ukizidi kuongezeka.
Angalau mawaziri wanne wanashikiliwa na wanajeshi ambao hawajafahamika muda mfupi kabla ya alfajiri ya Jumatatu.
Ripoti moja inasema waziri Mkuu Abdallah Hamdok pia alikamatwa , ingawa bado haijathibitishwa.
Haijafahamika bado ni kina nani hasa wanaotekeleza ukamataji huo. Jeshi la nchi hiyo halijasema lolote mpaka sasa.
Vyombo vya habari vinasema kwamba wanajeshi wasiotambulika wameizingira nyumba ya waziri mkuu Abdalla Hamdok .
Runinga ya Al Hadath inaripoti kwamba wanajeshi wamewakamata mawaziri wanne na mwanachama mmoja wa serikali ya mpito kulingana na vyanzo ambavyo havijatambuliwa.
Reuters pia imeripoti kwamba wanajeshi walivamia nyumba ya mshauri wa masuala ya habari wa waziri mkuu na kumkamata mapema Jumatatu.
Hali haijatulia Sudan, mvutano wa kisiasa umeingia katika sura nyingine tofauti
Muungano wa Wataalamu nchini humo umewataka raia kuingia barabarani ili kufanya maandamano kwa lengo la kuzuia mapinduzi hayo ya kijeshi. Kundi la watu wanaounga mkono demokrasia pia, wametoa wito wa wafuasi wao na wanaounga mkono demokrasia kutokubali mapinduzi yoyote ya kijeshi.
Mitandao kuzimwa
Hatua hiyo inajiri huku kukiwa na ripoti kuhusu kuzimwa kwa huduma ya mtandao nchini humo.
Mashuhuda wanasema mitandao haipatikani katika mji mkuu wa nchi hiyo, Khartoum, wakati kukiwa na picha za watu wenye hasira zikisambaa kwenye mitandao wakionekana kuchoma matairi mtaani.
Wanajeshi wamepelkwa mtaani kwenye jiji hilo, likizuia watu kutoka sehemu moja kwenda nyingine, mmoja wa mashuhuda aliiambia Reuters.
Uwanja wa ndege wa Khartoum sasa umefungwa, huku safari za ndege za kimataifa zikihairishwa
0 Comments