Header Ads Widget

WAONYWA KUTOCHAFUA PAMBA ILI KULINDA UBORA NA VIWANDA.

 Mashine za kuchambua Pamba Kiwanda cha NGS mjini Bariadi.


Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.


WAKULIMA wa Pamba pamoja na wadau wengine kwenye mnyororo wa thamani wa zao la Pamba ikiwemo vyama vyama vya ushirika (Amcos), wameonywa kuacha tabia ya kuchafua Pamba ili kulinda soko na Ubora wa zao hilo.


Aidha wamesisitizwa kuwa Pamba itakayonunuliwa katika msimu huu, ni Ile ambayo haijachanganywa na kitu chochote ikiwemo mchanga, Maji, mawe na takataka zingine ili kuendelea kulinda Ubora na thamani ya Pamba ya Tanzania na kwamba Uchafuzi huo huharibu mashine Viwandani.


Hayo yamebainishwa na Mkaguzi wa Viwanda kutoka Bodi ya Pamba Tanzania (TCA), Mhandisi Ramadhan Dissa wakati akikagua viwanda vya Pamba ambavyo vinafanyiwa matengenezo kwa ajili ya maandalizi ya uchambuaji wa Pamba katika msimu wa pamba 2025/2026, huku ikisisitizwa kuwa Ubora wa Pamba utasimamiwa tangu shambani, sokoni mpaka viwandani.


Mhandisi Dissa amesema Uchafuzi wa Pamba unasababisha hasara kubwa viwandani na kuongeza matumizi ya vipuri jambo ambalo ni hasara na pia Uchafuzi huo inashusha uwiano wa Pamba na mbegu (GOT) na kusababisha bei ya pamba kushuka.


"Mbegu zilizowekewa Maji zinakuwa na uotaji hafifu, uzalishaji wa Mafuta kuwa madogo na Mashudu kupata fangasi...wakulima wote na wengine tuzingatie kununua Pamba siyochanganywa na takataka yoyote ili kulinda thamani na Ubora wa Pamba ya Tanzania." Amesema.


Amesema kupitia ukaguzi huo, wanatoa Ushauri ili kumlinda mnunuzi wa Pamba aweze kuzalisha kwa kupata faida huku akifafanua kuwa katika ukaguzi huo wamebaini Viwanda vyote vimezingatia viwango na kukidhi maelekezo ya Bodi ya Pamba.



"Tumefanya matengenezo vipuri na magari ili kuanza ununuzi wa Pamba....kwenye Ubora tunashirikiana na wadau kuhakikisha zao linakuwa na Ubora pindi linapoingia kwenye Kiwanda, Pamba ikichafuliwa inasababisha gharama ya kuchambua, matengenezo tunayafanya kila wiki kutokana na Uchafuzi wa Pamba kwa kutumia hela nyingi" amesema Meneja huyo.



Meneja Mkuu wa Kampuni ya NGS, Sospeter Magese amesema wameshaanza kufanya maandalizi ya matengenezo ya mashine kwenye Kiwanda chao ili wachambue Pamba kupata mbegu na nyuzi.


Amesema matengenezo hayo ni moja ya maandalizi kwa ajili ya msimu wa 2025/2026 ambapo wanaondoa spea zilizoharibika na kuweka mpya Kwa ajili ya kuchambua Pamba ya wakulima.


Kwa upande wake Meneja wa kiwanda cha Alliance Ginneries, Boaz Ogolla ambaye pia ni Katibu wa Chama Cha Wanunuzi wa Pamba (TCA), amesema maandalizi ya ununuzi na uchambuaji wa Pamba yamekamilika huku akiwahakikishia wakulima wa Pamba kuwa watanunua Pamba yote iliyozalishwa nchini.


Amewataka wakulima hao kutunza Ubora wa Pamba ili kulinda soko la ndani na la kimataifa, na kwamba Mkakati wa BBT umechangia kupata Pamba safi ambayo imesimamiwa tangu ikipandwa hadi uvunaji.


"Mwaka jana uchafuzi ulikuwa mkubwa sana, lakini sasa tunaipongeza serikali na vijana wa BBT waliotoa Elimu kwa Wakulima, hivyo tunakwenda kujivunia juu ya uwekezaji huu" amesema Ogolla 


Afisa Ugani wa BBT, Mary Amani anayesimamia wakulima wa Kijiji cha Mkuyuni, amesema wamewaandaa wakulima na kuwapa Elimu juu ya namna Bora ya kuvuna ili kulinda Ubora pia kutunza Pamba kabla hawajapeleka sokoni.


Limbu Dedede, mkulima wa Pamba kijiji cha Mkuyuni amewashukuru Maafisa Ugani ambao wametoa Elimu pia wamewapatia viuatilifu kwa wakati na kwamba wanatarajia kupata mavuno ya kutosha.


Mwisho.


Mafundi wakitengeneza mashine za kuchambua Pamba kwenye Kiwanda cha NGS mjini Bariadi.


Mkaguzi wa Viwanda kutoka Bodi ya Pamba Tanzania (TCA), Mhandisi Ramadhan Dissa (kulia), akimwelekeza fundi wa Kiwanda cha NGS namna ya kutengeneza rola, kushoto ni Meneja wa NGS, Sospeter Magesa.




Mkaguzi wa Viwanda kutoka Bodi ya Pamba Tanzania (TCA), Mhandisi Ramadhan Dissa (katikati), akimwelekeza fundi wa Kiwanda cha NGS namna ya kutengeneza rola, kushoto ni Meneja wa NGS, Sospeter Magesa.


Mkaguzi wa Viwanda kutoka Bodi ya Pamba Tanzania (TCA), Mhandisi Ramadhan Dissa wakati akizunguma na waandishi wa Habari (hawapo pichani) mara baada ya kumaliza ukaguzi wa Kiwanda Cha NGS mjini Bariadi, ukaguzi huo ni sehemu ya maandalizi ya msimu wa pamba 2025/2026.


Afisa Ugani wa BBT, Mary Amani anayesimamia wakulima wa Kijiji cha Mkuyuni, akiongea na waandishi wa Habari (hawapo pichani) namna walivyotoa Elimu kwa Wakulima wa Pamba ili kuongeza tija na kupata Pamba safi.











Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI