Header Ads Widget

MBOZI KUIBADILI STENDI YA MALORI KUWA KARIAKOO

Na Moses Ng’wat, Mbozi

HALMASHAURI ya Wilaya ya Mbozi inapanga kujenga kituo cha biashara cha kimataifa katika eneo la Stendi ya Malori ya Vwawa,  kwa lengo la kuifanya wilaya hiyo kuwa kitovu cha biashara za kikanda.

Mradi huo utatekelezwa kwa mfumo wa ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP), huku wawekezaji kadhaa wakitajwa kuwa tayari wameanza michakato ya uwekezaji.

Hayo yalibainishwa na Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Maarifa Mwashitete, katika mahojiano maalumu yaliyofanyika Oktoba 12, 2026, siku chache baada ya Halmashauri kutoa notisi  kwa wafanyabiashara waliopo kuondoa biashara zao katika eneo hilo.

Alisema kituo hicho kinalengwa kuwa ‘Kariakoo Mpya’ ya Ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), kitasaidia kupunguza ulazima wa wafanyabiashara kutoka nchi jirani, hasa Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kusafiri hadi Kariakoo, Dar es Salaam, kutafuta bidhaa.

Kwa mujibu wa Mwashitete, kituo hicho kitakapokamilika, wafanyabiashara hao wataweza kupata huduma za kibiashara Vwawa, hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa bidhaa na kuimarisha biashara zinazovuka mipaka.

Alifafanua kuwa tayari wawekezaji kadhaa wameanza michakato ya uwekezaji katika mradi huo, ingawa hakubainisha majina yao wala thamani ya uwekezaji unaotarajiwa.

Akizungumzia maandalizi ya eneo hilo, Mwashitete alisema Halmashauri imesitisha ukusanyaji wa ushuru kwa wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao hapo na tayari wamepewa taarifa kuhusu hatua hiyo, ili kupisha utekelezaji wa mradi huo.

Alisema uamuzi huo unalenga kuwezesha maandalizi ya ujenzi bila kuwapa wafanyabiashara sababu ya kulalamika.

“Tulishaacha kukusanya ushuru, mwaka unaisha, kwa hiyo hakuna mtu atakayelalamika,  lengo ni kwenda kujenga na kulitengeneza eneo hilo kuwa kitovu cha biashara na kuwezesha zile biashara zinazopatikana Kariakoo zipatikane hapo,” alisema.

Mwashitete aliongeza kuwa kituo hicho cha biashara kinatarajiwa kuwa chanzo cha kudumu cha mapato kwa Halmashauri hiyo, sanjari na kuchochea shughuli za kiuchumi katika eneo hilo.Aidha, Mwashitete alisema 

Wafanyabiashara wanaoendesha shughuli zao katika eneo hilo wanatarajiwa kuhamishiwa Soko Kuu la Mjini Vwawa ili kuwawezesha kuendelea na shughuli zao za kujipatia kipato.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI