Na Angel Magesa (UoI), Matukio Daima Media, Iringa
CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT) kimeendesha mafunzo kwa walimu wenye ulemavu mkoa wa Iringa, yakilenga kuwawezesha kutumia mifumo ya kidijitali katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mafunzo hayo yaliyofanyika katika Ukumbi wa VETA mjini Iringa, yalihusisha matumizi ya mifumo mbalimbali, ikiwemo ya kujifunzia kwa njia ya mtandao, kupandishwa vyeo na kuomba uhamisho wa watumishi.
Mafunzo hayo ni mwendelezo wa mafunzo yanayoendelea kutolewa ikiwa ni hatua ya kuhakikisha walimu wenye ulemavu hawabaki nyuma katika matumizi ya teknolojia na wanapata fursa sawa za kutekeleza majukumu yao kama walimu wengine.
Kaimu Rais wa CWT, Mwalimu Shaban Ambindwile, alisema kuwawezesha walimu wenye ulemavu kutumia mifumo ya kidijitali ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya Taifa.
“Lazima tuwasaidie walimu wenye ulemavu ili waweze kuendana na dira ya maendeleo ya nchi. Wasipokuwa ndani ya mifumo ya utendaji, watabaki nyuma na hawataweza kuchangia kikamilifu katika kufanikisha dira hiyo,” alisema Ambindwile.
Alisema CWT iliamua kutumia sehemu ya michango ya wanachama wake kuendesha mafunzo hayo katika maeneo mbalimbali nchini, baada ya kubaini changamoto zinazowakabili walimu wenye ulemavu katika matumizi ya mifumo ya kidijitali.
Kwa upande wake, Clesensia Lwambano, mwalimu kutoka Shule ya Sekondari Lugalo, alisema mafunzo hayo yaliwasaidia walimu wenye changamoto za kuona na aina nyingine za ulemavu kuelewa namna ya kutumia mifumo ya kiteknolojia katika kazi zao.
“Tunashukuru kwa kutambua kundi hili, kwa sababu kabla ya mafunzo ilikuwa changamoto kwa baadhi yetu kutumia mifumo hiyo. Tunaamini mafunzo haya yatatusaidia kushiriki vizuri katika utekelezaji wa majukumu yetu,” alisema Lwambano.
Mwalimu Leo Sambara kutoka Shule ya Sekondari Mawelewele alisema mafunzo hayo yatawasaidia walimu wenye ulemavu kutumia mifumo ya Serikali katika kushughulikia masuala mbalimbali ya kiutumishi, yakiwemo kupandishwa vyeo na kuomba uhamisho.
“Sisi watumishi wenye ulemavu tunataka kupata haki sawa na watumishi wengine. Tunapoenda sambamba na maendeleo ya sayansi na teknolojia, matumizi ya mifumo ni muhimu. Mafunzo haya yatatusaidia kutekeleza majukumu yetu tukiwa katika vituo vya kazi,” alisema Sambara.
Aidha, Ambindwile alisisitiza umuhimu wa kudumisha amani nchini, akisema walimu na jamii kwa ujumla wana wajibu wa kuilinda na kuitangaza.
Alisema watu wenye ulemavu wanaweza kuathirika zaidi amani inapovurugika kutokana na changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo, zikiwemo za usafiri na uhamaji.

.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)




0 Comments