Header Ads Widget

CCM YATOA KAULI KUKWAMA MRADI WA KITUO CHA AFYA RUKOMA

Na Fadhili Abdallah, Kigoma 

Kamati ya siasa ya Chama  Cha Mapinduzi (CCM) mkoa Kigoma imeitaka serikali ya mkoa Kigoma kuisimamia  Halmashauri ya wilaya Uvinza ili  kukamilisha mradi wa kituo cha afya cha Rukoma kata ya Igalula Wilaya ya Uvinza  ambacho kimeshindwa kukamilika licha ya kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 560 kutumika.

Mwenyekiti wa CCM mkoa Kigoma,Jamal Tamim akiongoza wajumbe kamati hiyo alisema kuwa Waziri Mkuu Mstaafu, Kassim Majaliwa alishawahi kutoa maelekezo ya kituo hicho kukamilika na kuanza kutoa huduma lakini maelekezo hayo hadi sasa  hayajatekelezwa.

Tamim alisema kuwa kiasi cha shilingi milioni 546 zimetumika hadi sasa kiasi ambacho pia kimetolewa kwa vituo vingine vya afya ambavyo vimekamilika na kuanza kutoa huduma lakini kituo hicho kilichoanza kupokea fedha mwaka 2021 hadi sasa kimefikia aslimia 85 na hakuna dalili zozote za kituo hicho kuanza kutoa huduma karibuni.

Kwa upande Katibu wa CCM mkoa Kigoma, Christopher Pallangyo alisema kuwa vituo vilivyopata fedha kama hicho vicenza kutoa huduma lakini wanashangazwa na kituo hicho kimeshindwa kutoa hata huduma za nje wakati taratibu nyingine zikiendelea.

Kutokana na hilo alisema kuwa watapeleka maelekezo yao kwa Mkuu wa mkoa Kigoma,Balozi Simon Sirro Oktoba Mosi mwaka huu wakati wa majumuisho ya ziara hiyo kwa wilaya zote lakini alibainisha kuwa chama kimesikitishwa kwa kituo hicho cha afya kushindwa kufanya kazi hadi sasa.

Akitoa ufafanuzi kuhusiana na utekelezaji wa mradi huo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Uvinza, Masumbuko Kechegwa alisema kuwa  kuwa hadi sasa kiasi cha shilingi milioni 546 kimeshatumika kwa ajili ya mradi huo na kubainisha kwamba changamoto za usafirishaji vifaa, na kupanda kwa gharama ya vifaa vya ujenzi vimechangia mradi huo kushindwa kukamilika lakini jitihada zinafanyika kuhakikisha utoaji huduma inaanza hata kwa huduma ya wagonjwa wa nje (OPD).

Akizungumza katika ziara hiyo Mkuu wa wilaya Uvinza, Dinna Mathaman alionyeshwa kusikitishwa na utoaji huduma kituoni hapo kutoanza hadi leo wakati binafsi aliwaahidi wananchi hao huduma kuanza kutolewa Septemb Mosi mwaka huu na kwamba watalifanyia kazi suala hilo kwa mamlaka zinazohusika ili mradi ukamilike na utoaji huduma uanze.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI