Header Ads Widget

WAZAZI WATAJWA KUWA NA NAFASI KUBWA KUDHIBITI MIMBA ZA MABINTI

Na Angel Magesa (UoI), Matukio Daima Media

IRINGA. Wazazi wametakiwa kuongeza ukaribu na watoto wao wa kike na kuwapa elimu sahihi ya afya ya uzazi ili kupunguza mimba zisizotarajiwa miongoni mwa mabinti.

Ukosefu wa mawasiliano ndani ya familia, elimu duni kuhusu afya ya uzazi na ukatili wa kijinsia umetajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia tatizo hilo.

Akizungumza na Matukio Daima Media, Ofisa Maendeleo ya Jamii, Irene Samora, amesema baadhi ya mabinti huingia katika mahusiano bila kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu madhara na majukumu yanayoweza kutokana na mahusiano hayo, hali inayoweza kusababisha ujauzito.

Amesema elimu kwa watoto inapaswa kuanza mapema, hasa wanapoanza kubalehe, ili waweze kuelewa mabadiliko ya miili yao na namna ya kujilinda.

“Wazazi wana wajibu mkubwa wa kuwalinda watoto wao, kuwa karibu nao na kuwapa elimu. Mtoto anapofikia hatua ya kubalehe, mzazi anatakiwa kuzungumza naye kuhusu mabadiliko anayopitia,” amesema Irene.

Ameeleza kuwa wazazi wanapaswa kujenga mazingira yatakayowawezesha watoto kuzungumza kwa uhuru kuhusu changamoto wanazokutana nazo, badala ya kusubiri mpaka wapate ujauzito ndipo waanze kutafuta suluhisho.

Aidha, amesema shule na jamii zina nafasi muhimu ya kutoa elimu ya afya ya uzazi na kuwasaidia mabinti kufanya maamuzi sahihi.

Kwa upande mwingine, amesema baadhi ya mabinti hukumbana na shinikizo la kifamilia na kijamii wanapopata ujauzito kabla ya kuolewa, hali inayoweza kuwafanya kuficha mimba au kutafuta njia zisizo salama za kuitoa.

Amesema jamii inapaswa kuwekeza zaidi katika elimu, ushauri na fursa za kiuchumi kwa vijana wa kike ili kupunguza mazingira yanayoweza kuwafanya waingie katika mahusiano hatarishi.

Naye Francis Godwin amesema ukosefu wa mawasiliano kati ya wazazi na watoto huwafanya baadhi ya mabinti kukosa taarifa muhimu kuhusu mahusiano na afya ya uzazi.

Amesema mzazi anaposhindwa kuzungumza na mtoto wake kwa wakati, mtoto anaweza kutafuta majibu kutoka kwa marafiki au watu wengine ambao huenda wasiwe na taarifa sahihi.

“Ni muhimu wazazi na watoto wawe na muda wa kuzungumza. Mtoto anapokuwa na swali au changamoto, awe na mtu wa karibu wa kumuuliza na kupata ushauri sahihi badala ya kutegemea taarifa zisizo sahihi kutoka kwa watu wengine,” amesema Francis.

Ameongeza kuwa baadhi ya vijana hutegemea mbinu ya kalenda bila kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu matumizi yake, hali inayoweza kuongeza uwezekano wa kupata mimba zisizotarajiwa.

Kwa upande wake, Angel Magesa amesema ukatili wa kijinsia, ikiwemo ubakaji, ni miongoni mwa sababu zinazoweza kusababisha mabinti kupata ujauzito bila ridhaa yao.

Amesema jamii inapaswa kuwa macho na kutoa taarifa kwa mamlaka husika inapobaini vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na wanawake.

“Tatizo hili linahitaji ushirikiano wa wazazi, shule, viongozi na jamii kwa ujumla. Tukiwapa watoto elimu, ulinzi na fursa za kujenga maisha yao, tutakuwa tumechukua hatua muhimu katika kupunguza mimba zisizotarajiwa kwa mabinti,” amesema Angel.

Ameongeza kuwa viongozi wa mitaa, shule na jamii kwa ujumla wanapaswa kushirikiana kuwalinda watoto wa kike dhidi ya vitendo vya ukatili na mahusiano yanayoweza kuwaweka katika hatari ya kupata mimba.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI