Na Fadhili Abdallah,Kigoma
UKOSEFU wa maji katika kituo cha afya Rusaba wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma umesababisha huduma za upasuaji kushindwa kufanyika kwa miaka miwili sasa tangu kukamilika kwa kituo hicho na kilichoanza kutoa huduma za nje (OPD)
Kaimu Mganga Mkuu wa wilaya Buhigwe, Yohana Milinde alisema hayo akitoa taarifa kwa kamati ya siasa ya CCM mkoa Kigoma iliyofanya ziara kutembelea na kukagua utekelezaji wa mradi huo ambao umegharimu kiasi cha shilingi milioni 770.
Milinde alisema kuwa baada ya kukamilika majengo ya kipaumbele katika utoaji huduma ikiwemo majengo ya wagonjwa wa nje, jengo la huduma za uzazi na jengo la upasuaji huduma nyingine zilianza lakini huduma ya upasuaji haijaweza kuanza kutokana na kutokuwepo kwa huduma ya maji hivyo jitihada zimefanyika kuwezesha huduma ya maji ipatikane ili huduma ya upasuaji iweze kufanyika.
Kaimu Mganga Mkuu huyo wa wilaya Buhigwe alisema kuwa wameshaandika kuomba fedha kwa wafadhili na wahisani mbalimbali ambao wameonyesha nia ya kusaidia jambo hilo lakini halmashauri imetenga fedha kwa ajili ya kusaidia kutatua changamoto hiyo lakini bado fedh hazijapatikana na kwa siku za karibuni bado huduma hiyo haitaweza kufanyika.
Kufuatia hali hiyo Mwenyekiti wa CCM mkoa Kigoma,Jamal Tamim alisema kuwa atawasiliana na Waziri wa maji, Jumaa Aweso na Waziri wa Afya ili kuona namna changamoto hiyo inavyoweza kutatuliwa.
Hata hivyo Mwenyekiti huyo na wajumbe wake wamesema kuwa licha ya changamoto hiyo lakini wamepongeza kuanza kutolewa kwa huduma za matibabu katika kituo hicho cha afya na hivyo kusogeza huduma kwa wananchi akilinganisha na kituo cha afya Rukoma wilaya ya Uvinza ambacho licha ya kutumia Zaidi ya milioni 560 lakini haijulikani huduma zitaanza lini.










0 Comments