Na Elamu Nyaulingo (UOI) Matukio Daima Media, Iringa
Baadhi ya wananchi mkoani Iringa wameeleza uelewa wao kuhusu tatizo la udumavu kwa watoto na namna wanavyoweza kujikinga, wakitaja ulaji wa lishe bora na kuwapatia watoto chakula kwa wakati kuwa miongoni mwa hatua wanazozitumia katika familia zao ili kusaidia ukuaji na maendeleo ya watoto.
Wananchi hao, waliozungumza na Matukio Daima Media kuhusu uelewa wao juu ya udumavu, wameeleza kwa mitazamo tofauti kuwa tatizo hilo linahusishwa na mtoto kutopata lishe bora na virutubisho muhimu vinavyohitajika katika ukuaji, huku wakisisitiza umuhimu wa wazazi kuzingatia aina ya vyakula wanavyowapatia watoto.
“Udumavu, ninavyoelewa mimi, ni mtoto ambaye amekosa lishe,” amesema Fatuma Kinyaga, mkazi wa Kitwiru, wakati akieleza namna anavyojitahidi kuhakikisha watoto wake wanapata chakula chenye mchanganyiko wa virutubisho.
Fatuma amesema katika familia yake amekuwa akizingatia matumizi ya vyakula mbalimbali, ikiwemo mboga za majani, dagaa, karoti, nyama, maharage na mayai, akiamini kuwa mchanganyiko huo unasaidia kuwapatia watoto lishe inayohitajika katika ukuaji wao.
Amesema wazazi, hususan kina mama, wanapaswa kuzingatia muda wa kuwapatia watoto chakula na kuhakikisha milo yao ina vyakula vya aina mbalimbali badala ya kutegemea aina moja ya chakula.
“Wamama wengine nawashauri waangalie watoto, wawapikie watoto kwa wakati na wazingatie chakula kwa wakati,” amesema Fatuma.
Ametaja watoto wake kuwa ni Yustafa Shafii Umbi na Warda Shafii Umbi, huku akieleza kuwa amekuwa akijitahidi kuwapatia vyakula tofauti kwa lengo la kuhakikisha wanapata lishe kamili
Kwa upande wake, Jestina Doris, ambaye pia alizungumza kuhusu uelewa wake wa udumavu, amesema anaelewa tatizo hilo kuwa linaweza kumpata mtoto anayekosa chakula chenye lishe bora na virutubisho vinavyohitajika katika ukuaji wake.
“Udumavu mimi ninavyoelewa, labda ni kwa mtoto kukosa chakula, yaani lishe bora,” amesema Jestina.
Amesema njia anayotumia katika familia yake ni kuhakikisha mtoto anapata chakula kwa wakati, huku akitaja baadhi ya vyakula anavyompatia kuwa ni ugali, wali na dagaa pamoja na vyakula vingine vinavyoliwa na familia.
“Nitampatia tu chakula, maana yake ni kumpatia chakula kwa wakati. Mimi namtengenezea ugali, wali na dagaa, yaani chakula ambacho naona tunachokula sisi,” amesema Jestina.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), udumavu ni hali ya mtoto kuwa na kimo kifupi kulinganisha na umri wake kutokana na utapiamlo wa muda mrefu au unaojirudia. WHO inaeleza kuwa tatizo hilo huhusishwa na sababu mbalimbali, zikiwemo lishe duni, afya na lishe duni ya mama, magonjwa ya mara kwa mara pamoja na namna isiyofaa ya ulishaji na malezi katika hatua za mwanzo za maisha ya mtoto.
WHO inaeleza kuwa kinga dhidi ya utapiamlo na udumavu inahitaji lishe bora ya mama kabla na wakati wa ujauzito na kipindi cha kunyonyesha, unyonyeshaji unaofaa, vyakula vya nyongeza vilivyo salama na vyenye mchanganyiko wa virutubisho, pamoja na upatikanaji wa huduma za afya, maji safi, usafi wa mazingira na usafi binafsi






0 Comments