![]() |
| Wananchi katika mkutano huo September 18, 2026,Mtaa wa Mbwamaji |
Na Mwandishi Wetu, Kigamboni
Wananchi wa Mtaa wa Mbwamaji, Kata ya Somangila, Wilaya ya Kigamboni wameazimia kujenga Shule ya Msingi kwa nguvu zao wenyewe baada ya kukosa shule mbadala kwa miaka minne.
Uamuzi huo umefikiwa katika mkutano mkuu wa Serikali ya Mtaa huo September 18,2026 ambapo wananchi wamekubaliana kila kaya kuchangia Shilingi 15,000 na kushirikisha wadau wa ndani na nje ya mtaa.
Mtaa wa Mbwamaji ulikuwa na shule ya msingi iliyojengwa na wananchi mwaka 1964, na Serikali iliongeza majengo mawili na kufanya ukarabati mwaka 1992. Shule hiyo ilihamishwa mwaka 2022 kwenda Mtaa wa Kizani kupisha ujenzi wa Soko la Samaki.
Tangu wakati huo wananchi wanasema wamekuwa wakifuatilia kupitia ofisi ya mtaa bila mafanikio, huku watoto wakilazimika kutembea umbali mrefu na kukumbana na changamoto njiani.
![]() |
| Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Mbwamaji, Mhe. Yohana Luhemeja 'Maziku'. |
Mwenyekiti wa Mtaa huo, Mhe. Yohana Luhemeja 'Maziku' amesema wamepokea michoro ya madarasa mawili kutoka Manispaa ya Kigamboni, ambapo kila darasa linakadiriwa kugharimu Shilingi milioni 23, jumla ya milioni 46.
Amesema wameunda Kamati ya Ujenzi yenye wajumbe 15 itakayosimamiwa na Serikali ya Mtaa, na shule inatarajiwa kujengwa eneo la Uwanja wa Dung Farm.
"Kwa mujibu wa mpango, shule itakuwa na majengo saba na ofisi tatu za walimu. Kwa sasa tuna michoro ya madarasa mawili ya kisasa tutakayoanza kwa nguvu za wananchi, madarasa matano yaliyobaki tutaiomba Serikali itusaidie," amesema Maziku.
Aidha ameishukuru Serikali kwa ushirikiano ikiwemo upatikanaji wa eneo la ujenzi.
![]() |
| Mchoro wa ramani hiyo ya majengo mawili ya madarasa kwa Shule ya Msingi Mbwamaji |










0 Comments