Na Angel Magesa (UoI)Matukio Daima Media, Iringa
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Iringa lilitenga zaidi ya Sh milioni 43.6 kwa ajili ya kuboresha huduma ya umeme katika Kata ya Mwangata, Manispaa ya Iringa.
Fedha hizo zitatumika kuongeza nguvu ya umeme, kufunga transfoma na kuboresha miundombinu katika maeneo ambayo yamekuwa yakikabiliwa na changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara.
Taarifa hiyo ilitolewa na Ofisa Habari wa TANESCO Mkoa wa Iringa, Donasian John, kwa niaba ya Meneja wa shirika hilo mkoani hapa, wakati akijibu kero zilizowasilishwa na wananchi wa Mwangata.
Alisema mradi huo utahusisha uwekaji wa transfoma na vifaa vingine vitakavyoongeza uwezo wa mfumo wa umeme na kuboresha upatikanaji wa huduma hiyo.
Alisema ongezeko la watumiaji wa umeme pamoja na matumizi makubwa ya vifaa na mashine za umeme limeongeza mahitaji ya nishati katika maeneo mbalimbali ya kata hiyo.
Kutokana na hali hiyo, alisema TANESCO ilikuwa ikiendelea kuchukua hatua za kuongeza nguvu ya umeme ili kukidhi mahitaji ya wananchi na kuimarisha shughuli za kiuchumi.
Kero hiyo iliwasilishwa katika mkutano wa wananchi uliohudhuriwa na Mbunge wa Iringa Mjini, Fadhili Fabian Ngajilo, ambapo wakazi walipata nafasi ya kueleza changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Akizungumza baada ya kusikiliza majibu ya TANESCO, Ngajilo alilipongeza shirika hilo kwa kufika mbele ya wananchi, kusikiliza malalamiko yao na kuja na ufumbuzi wa changamoto ya umeme iliyokuwa ikiwakabili kwa muda mrefu.
Alisema hatua ya TANESCO kutenga fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya umeme ilikuwa habari njema kwa wananchi wa Mwangata, hususan wafanyabiashara na wajasiriamali wanaotumia mashine zinazohitaji nguvu kubwa ya umeme.
“Nalipongeza TANESCO kwa kusikiliza kilio cha wananchi na kuja na majibu yenye ufumbuzi. Kutengwa kwa fedha hizi kutasaidia kuboresha huduma ya umeme na kuwawezesha wananchi kuendelea na shughuli zao za kiuchumi bila kukumbwa na tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara,” alisema Ngajilo.
Mbunge huyo pia alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwa karibu na wananchi, kusikiliza changamoto zao na kuhakikisha fedha za kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo zinatolewa kwa wakati.
Alisema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuonesha dhamira ya dhati ya kutatua changamoto za wananchi kupitia utekelezaji wa miradi ya umeme, maji, afya, elimu na miundombinu mingine muhimu.
“Tuna kila sababu ya kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwa karibu na changamoto za wananchi na kuhakikisha fedha za miradi zinatolewa kwa wakati. Fedha hizi za kuboresha umeme Mwangata ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuwaletea wananchi maendeleo,” alisema Ngajilo.
Alisema upatikanaji wa umeme wa uhakika utasaidia kuongeza uzalishaji, kukuza biashara, kuongeza ajira na kuboresha maisha ya wananchi wa Mwangata na maeneo mengine ya Manispaa ya Iringa.TAZAMA VIDEO BOFYA HAPA
Ngajilo aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa TANESCO wakati wa utekelezaji wa mradi huo, huku akisisitiza umuhimu wa kazi hiyo kutekelezwa kwa wakati na kwa kiwango kilichokusudiwa ili wananchi waanze kunufaika.
Awali, wananchi wa Mtaa wa Bombambili walilalamikia kukatika kwa umeme mara kwa mara, hali ambayo walisema ilikuwa ikiathiri shughuli zao za uzalishaji, hususan matumizi ya mashine zinazohitaji nguvu kubwa ya umeme.
Mkazi wa eneo hilo, Athuman Mrimbo, alisema kulikuwa na mashine tatu zinazohitaji umeme wenye nguvu kubwa, lakini zilipowashwa umeme ulikatika na kusababisha shughuli zao kusimama.
“Tuliomba TANESCO ituongezee nguvu ya umeme kwa sababu mashine hizi zinahitaji umeme mkubwa. Tulipoziwasha, umeme ulikatika na shughuli zetu kusimama,” alisema Mrimbo.
Alisema maofisa wa TANESCO walifika mara kadhaa kukagua hali ya umeme katika eneo hilo, lakini tatizo liliendelea licha ya wananchi kutoa taarifa.
Wananchi waliiomba TANESCO kufunga transfoma yenye uwezo mkubwa ili kukidhi ongezeko la mahitaji ya umeme na kupunguza kukatika kwa huduma hiyo.
TANESCO ilieleza kuwa changamoto hiyo ilisababishwa na ongezeko la matumizi ya umeme, pamoja na vifaa na mashine zinazotumiwa na wananchi kuhitaji nguvu kubwa kuliko uwezo wa miundombinu iliyopo.


.jpeg)
.jpeg)






0 Comments