Na Matukio Daima Media, Kilosa
MGOGORO wa ardhi unaodaiwa kudumu kwa miaka kadhaa kati ya wananchi wa Kijiji cha Kitete Msindazi, Kata ya Ruhembe wilayani Kilosa, Mkoani Morogoro na Hifadhi ya Taifa ya Mikumi umechukua sura mpya baada ya Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka, kufika katika eneo linalolalamikiwa na kuahidi kuanza upya mchakato wa kutafuta suluhu.
Wananchi wa kijiji hicho wamekuwa wakidai utekelezaji wa maamuzi yaliyowahi kufikiwa na Serikali katika kushughulikia migogoro ya ardhi kati ya vijiji vinavyopakana na hifadhi, wakisema pamoja na baadhi ya vijiji kunufaika na hatua zilizochukuliwa, wao bado hawajaona utekelezaji wa jambo hilo katika eneo lao.
Wananchi hao wanasema changamoto hiyo imewaacha bila maeneo ya kutosha ya kilimo, huku eneo linalohusishwa na mgogoro likiwa halitumiki rasmi na wananchi, lakini likiendelea kulindwa na askari wa Hifadhi ya Taifa ya Mikumi.
Kwa mujibu wa wananchi hao, miongoni mwa maeneo yaliyowahi kufanyiwa uhakiki ni Kijiji cha Kitete Msindazi, ambapo wanadai takribani hekta 4,972 zilihusishwa na eneo la hifadhi na kwamba hatua zilizofuata zilipaswa kuweka wazi hatima ya eneo hilo na matumizi yake.
Athuman Abdi Kihombe, ambaye alijitambulisha kuwa aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Mpango wa Matumizi ya Ardhi wa Kijiji hicho na Mratibu wa Mbunge wa Mikumi wa wakati huo, Abdulsalaam Suleiman Ameir maarufu kama SAS amesema suala hilo limefuatiliwa kwa muda mrefu katika ngazi mbalimbali bila wananchi kupata utekelezaji waliokuwa wakiutarajia.
Kihombe alikwenda na nyaraka alizozisoma mbele ya Mkuu wa Wilaya, akieleza kuwa mwaka 2011 Waziri wa Maliasili na Utalii wa wakati huo, Ezekiel Maige, alitoa majibu Bungeni kuhusu mipaka ya Hifadhi ya Taifa ya Mikumi baada ya swali la Mbunge wa Mikumi wa wakati huo, SAS.
Kihombe amesema baada ya wananchi kuona utekelezaji wa maamuzi hayo unasuasua, walimfuata aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi,na kupitia timu ya mawaziri nane wa kushughulikia migogoro ya ardhi kati ya wananchi na maeneo ya hifadhi, timu maalum iliundwa katika wilaya hiyo kwa kushirikisha wananchi, wataalamu wa ardhi na wawakilishi wa Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, ambapo uhakiki wa mipaka ulifanyika na alama zikawekwa katika maeneo yaliyohusika.
Cloud Petter, mkazi wa Kitete Msindazi, amesema changamoto kubwa kwa sasa ni uhaba wa maeneo ya kulima wakati kuna eneo ambalo wananchi wanaamini lilipaswa kufanyiwa uamuzi wa mwisho badala yake wanaona maeneo hayo yanalindwa na askari wa hifadhi bila wananchi wanaotegemea kilimo kwa maisha yao wakishindwa kuyatumia.
Cloud katika mkutano wa hadhara wa Kijiji, akamuomba mkuu wa Wilaya ya Kilosa kwenda eneo linalolalamikiwa na kujionea hali halisi ili kupata picha halisi ya changamoto inayowakabili wananchi.
Kwa upande wake, Ismail Ngwale, mkazi wa Kitete Msindazi, amesema wananchi wamekuwa wakisubiri majibu ya Serikali kwa muda mrefu na kwamba suala hilo linahitaji hatua inayoweza kuleta utulivu wa kudumu katika kijiji hicho.
Wananchi waliohudhuria mkutano huo walionyesha matumaini baada ya Mkuu wa Wilaya kukubali kwenda katika eneo walilokuwa wakilalamikia, huku baadhi yao wakisema hatua hiyo imewapa picha kwamba Serikali italifanyia kazi shauri hilo kwa kuwa umeona uhalisia
Baadhi ya wananchi walionekana kushangilia huku wengine wakijilaza mbele yake kama ishara ya kumshukuru kwa kukubali kusikiliza kilio chao na kwenda kujionea hali halisi, huku wengine wakicheza muziki kwa Furaha.
Aliporudi eneo la mkutano, Mkuu huyo wa wilaya alitaka kwanza kusikia sauti za wananchi ambapo Mwenyekiti mstaafu wa Kijiji cha Kitete Msindazi, Timilai Lunyungu, amesema baada ya kufika eneo hilo wamejiridhisha kuwa suala hilo linahitaji utulivu na hatua za Serikali badala ya wananchi kuendelea kuingia katika maeneo yenye mgogoro hivyo kuwasihi wananchi watulivu wakati Serikali ikiendelea na mchakato kulishughulikia suala hilo.
Naye Diwani wa Kata ya Ruhembe, Frank Hamis , akasema wananchi wanapaswa kuendelea kuwa watulivu ili Serikali iweze kupata nafasi ya kulishughulikia suala hilo kwa utaratibu.
Hata hivyo diwani huyo ameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuruhusu mazao ambayo tayari yamepandwa katika eneo linalolalamikiwa, hasa mahindi yaliyokuwa karibu kuvunwa, yaachwe yakomae na kuvunwa badala ya kuondolewa mara moja.
Aidha akaomba wananchi waliokamatwa au wanaokabiliwa na mashauri kutokana na mgogoro huo waangaliwe kwa jicho la huruma na ikiwezekana mashauri yao yaondolewe kwenye vyombo vya Dola.
Akijibu ombi hilo, Shaka amesema Serikali imepokea hoja hiyo na itaishughulikia baada ya kushauriana na mamlaka husika, badala ya kutoa uamuzi wa moja kwa moja kuhusu mashauri yaliyo kwenye vyombo vya Dola.
Akawataka wananchi kutokwenda katika maeneo yenye mgogoro kufanya shughuli mpya za kilimo, ujenzi au maendeleo mengine wakati Serikali ikiendelea na mchakato wa kutafuta suluhu baada ya kuundwa kwa timu ya maridhiano itakayoshirikisha wawakilishi wa Wananchi, wataalamu,na wadau wengine.
Amesema Serikali ya wilaya imeona mgogoro huo unahusu maisha ya wananchi na kwamba haupaswi kuendelea bila kutafutiwa ufumbuzi.
“Mgogoro huu sio mkubwa kama ulivyokuwa ukitengenezwa. Sisi wenyewe Serikali ya wilaya tunaweza kuumaliza. Rais ametupa nyenzo zote za kufanyia kazi, tukishindwa hata kwa hili dogo tunamwangusha,” alisema Shaka.
Shaka amesema baadhi ya watu wamekuwa wakiufanya mgogoro huo uonekane mkubwa kuliko ulivyo, huku akisisitiza kuwa Serikali sasa inalenga kuufanyia kazi kwa hatua na taratibu ili pande zote ziwe salama, ziiishi kwa amani na utulivu na shughuli za uzalishaji ziendelee kama kawaida.
“Ufunguo wa suluhisho tunao, lakini tunataka utatuzi ufuate hatua na taratibu zote. La msingi na kubwa ni kuwa watulivu wakati suala hili linashughulikiwa,” akaongeza
Katika hatua nyingine, Shaka aliwapa muda wa mwezi mmoja wananchi wenye mazao yaliyopo katika eneo lenye mgogoro kuyaondoa, huku akisisitiza kuwa Serikali haitaruhusu watu wengine kuingia katika eneo hilo kwa ajili ya kuanzisha shughuli mpya na watakaokwenda kinyume watambue hawatafumbiwa macho na wataonekana ni wasiotaka mchakato wa kutafuta suluhu.
Mwisho








0 Comments