Na Matukio DaimaMedia
JEZI ya Taifa Stars imeibua mjadala baada ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, kuikosoa na kusema haipaswi kutetewa, bali kufanyiwa maboresho ili iwe na ubora unaokubalika.
Makonda amesema jezi hiyo si bidhaa ya kawaida kwa kuwa inawakilisha Tanzania kwa kubeba jina, bendera, rangi na taswira ya nchi katika mashindano ya kimataifa, hivyo inapaswa kuzingatia hadhi ya Taifa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, na waandishi wa habari Makonda amesema jambo la kwanza ni kuhakikisha jezi hiyo ina ubora unaokubalika na jambo la pili ni kuwepo kwa mpango mzuri wa uuzaji ili iweze kuwafikia wananchi.
“Jezi ni mbaya! Yaani sio suala la kumung'unya maneno, jezi ni mbaya!” alisema Makonda, akisisitiza kuwa hawezi kukubaliana na hoja za kuitetea jezi hiyo badala ya kuangalia namna ya kuiboresha.
Amesema kuwa, alianza kufuatilia suala hilo baada ya kutaka kufahamu namna jezi hiyo ilivyoandaliwa, kuidhinishwa, kuzinduliwa na kutangazwa, akitaka kujua kama taratibu na makubaliano yaliyowekwa zilifuatwa.
Sambamba na hilo, Makonda amesema baada ya kusoma mkataba kati ya TFF na Sandaland Fashion Wear Limited, aliibua maswali 22 kuhusu mambo mbalimbali, yakiwemo udhamini, usambazaji wa vifaa, malipo, haki za kibiashara na ubora wa jezi.
Ameongeza kuwa, miongoni mwa mambo yanayohitaji ufafanuzi ni aina ya mkataba huo, akitaka kujua kama ulihusu udhamini, usambazaji wa vifaa au mambo yote mawili. Mkataba huo pia una vipengele kuhusu matangazo, matumizi ya nembo na uuzaji wa bidhaa zenye nembo ya Taifa.
Aidha, Makonda alihoji kipengele kinachotaja vipimo vinavyotakiwa kwa jezi hiyo, akitaka kujua vipimo hivyo vimewekwa wapi, nani aliipima na nani alithibitisha kuwa imekidhi kiwango kilichowekwa.
Amesema kuwa, TFF kuidhinisha muonekano wa jezi hakumaanishi kuwa bidhaa iliyotengenezwa imekidhi ubora unaotakiwa, kwa kuwa kuangalia muonekano na kuthibitisha ubora wa bidhaa ni hatua mbili tofauti.






0 Comments