Header Ads Widget

MSALATO WAFIKIA ASILIMIA 89, KUKAMILIKA MWAKA HUU

 


Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma

UJENZI wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato mkoani Dodoma umefikia asilimia 89.02 kwa upande wa miundombinu, huku Serikali ikitarajia kukamilisha kazi hizo ifikapo Novemba 27, 2026, imeelezwa.

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta, amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo, akieleza kuwa ujenzi wa majengo umefikia asilimia 78.37 na unatarajiwa kukamilika Desemba 30, 2026.


Amesema mradi huo unatekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), ukiwa na lengo la kuimarisha miundombinu ya usafiri wa anga, kuongeza uwezo wa kuhudumia abiria na mizigo na kuimarisha mtandao wa usafiri wa anga kitaifa na kikanda.

Amesema Msalato ni miongoni mwa viwanja 12 ambavyo TANROADS inaendelea kusimamia ukamilishaji wake, baada ya Serikali mwaka 2024 kurejesha jukumu la ujenzi wa viwanja vya ndege kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TCAA), huku miradi iliyoanza chini ya TANROADS ikiendelea kukamilishwa na Wakala huo.


Mhandisi Besta amesema awamu ya kwanza ya ujenzi wa Msalato inatekelezwa kupitia mikataba miwili, ambapo Package One inahusu ujenzi wa miundombinu na Package Two inahusu ujenzi wa majengo.

"katika Package One, ujenzi wa njia ya kurukia na kutua ndege umefikia asilimia 98, njia za viungio (taxiways) asilimia 99 na eneo la maegesho ya ndege (apron) asilimia 99, huku barabara ya kuingia kiwanjani, barabara za ndani na maegesho ya magari zikifikia asilimia 75.," Amesema

Kwa mujibu wa Mhandisi Besta, mfumo wa maji umefikia asilimia 89, uzio na mageti asilimia 76, huku kazi za umeme pamoja na vifaa vya kuongozea ndege zikifikia asilimia 90, na kazi zilizobaki zikihusisha upandaji wa nyasi katika maeneo ya usalama, taa za kuongozea ndege, mabomba na tanki la maji pamoja na kukamilisha uzio na mageti.


Kwa upande wa Package Two, amesema ujenzi wa jengo la abiria umefikia asilimia 81, Mnara wa Kuongozea Ndege asilimia 74, Kituo cha Huduma za Zimamoto asilimia 88, vituo vya umeme asilimia 71 na jengo la huduma za hali ya hewa asilimia 87.


" Kazi zinazoendelea katika majengo hayo ni pamoja na umaliziaji, usimikaji wa mifumo ya mitambo, umeme na mabomba, ufungaji wa vifaa vya TEHAMA na mawasiliano, mashine za ukaguzi wa mizigo, madaraja ya kupitisha abiria, vifaa vya hali ya hewa na magari ya zimamoto, " Amesema

.

Mhandisi Besta amesema uwanja huo unajengwa kwa hadhi ya Daraja la 4E kwa viwango vya Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO), ukiwa na njia ya kurukia na kutua ndege yenye urefu wa mita 3,600 na upana wa mita 45, pamoja na mabega yenye upana wa mita 7.5 kila upande.


Amesema kwa uwezo huo, Msalato utaweza kuhudumia ndege kubwa aina ya Boeing 787 Dreamliner yenye uwezo wa kubeba abiria 350, huku kiwanja hicho kikiwa na uwezo wa kuhudumia abiria milioni 1.5 kwa mwaka na kuwezesha huduma za ndege wakati wa usiku na mchana.


Ameeleza kuwa kukamilika kwa mradi huo kunatarajiwa kuongeza fursa za biashara, uwekezaji, utalii, usafirishaji wa mizigo na ajira, pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Dodoma na Taifa kwa ujumla.


Kwa mujibu wa Mhandisi Besta, mradi huo tayari umezalisha ajira 9,059 kwa Watanzania katika kipindi cha utekelezaji, ambapo ajira 3,571 zimetokana na Package One na 5,488 kupitia Package Two, huku wafanyakazi wa kigeni wakiwa 47.


Ametoa wito kwa Watanzania, hususan wakazi wa Dodoma, kutumia fursa zitakazotokana na uwepo wa uwanja huo kukuza biashara, ikiwamo usafirishaji wa bidhaa zinazohitaji kufika sokoni kwa haraka kama matunda, mboga mboga, samaki, kuku na maua, pamoja na kutumia fursa katika sekta ya utalii.

Sambamba na maendeleo ya mradi huo, Mhandisi Besta ametoa tahadhari kuhusu uwezekano wa kutokea kwa hali ya El Niño kati ya Oktoba na Desemba 2026, akisema TANROADS inaendelea kukagua barabara, madaraja, makaravati na mitaro, kusafisha mifumo ya kupitisha maji na kujiandaa kwa mwitikio wa haraka katika maeneo yatakayokumbwa na athari za mvua kubwa, huku akiwataka wananchi kuchukua tahadhari na kukumbuka msemo wa “Kawia ufike.”


Mwisho

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI