Askofu wa kanisa la Romani Katoliki Jimbo la Iringa Romanus Mihali ambae alikuwa mgeni rasimi kwenye mahafali ya kidato cha nne Kigonzile Sekondari akimkabidhi cheti cha kuhitimu mwanafunzi Jimmy Edward Uphoro ,kulia ni mkurugenzi wa shule hizo Father Aidan Ulungi
Na Matukio Daima Media , Iringa
WAHITIMU wa Kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari Kigonzile, Manispaa ya Iringa, wamewapongeza wazazi na walezi wao kwa kujitoa kuwasomesha katika shule hiyo yenye mazingira mazuri ya kujifunzia, huku wakiahidi kufanya vizuri katika Mtihani wa Taifa.
Wakizungumza na Matukio Daima Media baada ya sherehe za mahafali zilizofanyika shuleni hapo jana, wahitimu Jimmy Edward Uphoro na Brian Baraka Mbangalala walisema wamejengwa vyema kielimu, kinidhamu na kimaadili katika kipindi chote cha miaka minne ya masomo yao.Walisema tangu walipojiunga na Kidato cha Kwanza hadi kuhitimu Kidato cha Nne, hawajawahi kujutia uamuzi wa wazazi wao wa kuwapeleka kusoma katika shule hiyo kutokana na malezi bora na ufundishaji wenye weledi walioupata.
Uphoro alisema walimu wa shule hiyo wamekuwa wakitimiza wajibu wao kwa uadilifu na kujenga uhusiano wa karibu na wanafunzi, hali iliyowapa uhuru wa kuuliza maswali na kuomba msaada kila walipokutana na changamoto za kitaaluma au kijamii.
Alisema mazingira hayo yaliwasaidia wanafunzi kuongeza bidii katika masomo, kupenda kujisomea na kuelewa kwamba ufaulu mzuri haupatikani kwa bahati, bali unatokana na nidhamu, juhudi, ushirikiano na matumizi sahihi ya muda.
“Walimu wetu wamekuwa marafiki wa karibu wa wanafunzi. Kila tulipokwama katika jambo fulani tuliweza kuwafuata, kuwauliza na kupata majibu pamoja na maelekezo yaliyotusaidia kuendelea na masomo yetu,” alisema Uphoro.
Aliongeza kuwa njia bora ya kuwashukuru wazazi wao ni kufanya vizuri katika mitihani, kuendelea kuwa na tabia njema na kulitunza jina la shule hata baada ya kumaliza masomo yao.“Kwa kujitolea kwa wazazi wetu kutusomesha hadi hapa tulipofika, zawadi kubwa tunayowaahidi ni kufanya vizuri katika Mtihani wa Taifa. Heshima kubwa kwa shule yetu ni sisi wahitimu kufaulu,” alisema.
Uphoro aliwashauri wazazi wanaotafuta shule zenye malezi bora, nidhamu na elimu yenye kiwango kizuri kuwapeleka watoto wao katika Shule ya Sekondari Kigonzile na Shule ya Msingi St. Dominic.
Kwa upande wake, mhitimu Brian Baraka Mbangalala alisema wana matumaini makubwa ya kufanya vizuri katika Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne kutokana na maandalizi waliyopata kutoka kwa walimu wao.
Aliomba wazazi, walezi na jamii kuendelea kuwaombea afya njema na mafanikio wakati wote wa maandalizi na kipindi cha kufanya mitihani yao.
Mbangalala alisema msaada wa wazazi haukuishia katika kulipa ada na michango mbalimbali, bali ulihusisha pia ushauri, maombi, ufuatiliaji wa maendeleo yao na kuwahamasisha kutokata tamaa walipokutana na changamoto.
Aliwahimiza wanafunzi wanaoendelea na masomo shuleni hapo kutumia vizuri nafasi waliyopewa, kuwaheshimu walimu, kusoma kwa bidii na kuepuka vitendo vinavyoweza kuhatarisha ndoto zao.
Awali, Mkurugenzi wa Shule za Kigonzile na St. Dominic, Padri Aidan Ulungi, alisema mafanikio yanayopatikana katika shule hizo yanatokana na ushirikiano mkubwa kati ya uongozi, walimu, wazazi, wanafunzi na wadau mbalimbali wa elimu.
Alisema wazazi wameendelea kuonesha imani kwa shule hizo kwa kuwapeleka watoto wao kupata elimu, huku walimu wakijitahidi kuhakikisha wanafunzi wanapata maarifa, nidhamu na misingi bora ya maisha.
Padri Ulungi alisema shule hizo zitaendelea kuimarisha mazingira ya kufundishia na kujifunzia ili kuwajenga wanafunzi wenye uwezo wa kujitegemea, kulitumikia taifa na kukabiliana na ushindani wa kielimu na kiteknolojia.
Mgeni rasmi katika mahafali hayo, Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Iringa, Romanus Mihali, aliwapongeza wazazi kwa kuendelea kuziamini shule hizo na kuwasihi kuwa mabalozi wa kuzitangaza kwa jamii.
Askofu Mihali alisema mafanikio ya taasisi za elimu yanahitaji ushirikiano wa wadau wote, hivyo akawaomba wananchi, waumini na wahitimu wa zamani kuendelea kuzisaidia shule hizo katika kuimarisha miundombinu na huduma za elimu.
Aliwataka waliosoma katika shule za St. Dominic na taasisi nyingine zinazosimamiwa na Kanisa kurejea na kutoa mchango wao kwa namna mbalimbali ili kuwasaidia wanafunzi wa sasa na vizazi vijavyo.
Vilevile, Askofu Mihali aliwapongeza walimu kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuwaandaa wanafunzi kitaaluma na kuwajengea misingi ya nidhamu, uadilifu, uwajibikaji na hofu ya Mungu.
Aliwahimiza wahitimu kutambua kwamba kumaliza Kidato cha Nne si mwisho wa safari yao ya elimu, bali ni hatua muhimu inayowaandaa kuingia katika ngazi nyingine za masomo na maisha.
Pia aliwataka kuepuka makundi yasiyofaa, matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii na tabia zinazoweza kuharibu malengo yao, huku akisisitiza umuhimu wa kusikiliza ushauri wa wazazi na walimu.
Aidha, Askofu Mihali alipongeza jitihada za Serikali ya Tanzania za kuendelea kuwekeza katika sekta ya elimu na kuiweka elimu miongoni mwa maeneo muhimu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Alisema kila mwananchi ana wajibu wa kushiriki katika utekelezaji wa dira hiyo kwa kuwa maendeleo ya taifa yanategemea uwepo wa jamii iliyoelimika, yenye maadili, ubunifu na uwezo wa kutumia maarifa kutatua changamoto.
Askofu Mihali alisema Kanisa Katoliki litaendelea kushirikiana na Serikali na wadau wengine katika kutoa elimu bora inayolenga kumjenga mwanafunzi kitaaluma, kiroho, kimwili na kimaadili.
TANGAZO LA SHULE

















0 Comments