TAASISI ya Uhifadhi na Urithi Tanzania (TCHI) imelaani vikali matukio ya kikatili ya kuuawa kwa simba kwa sumu katika eneo la Ndutu, Ngorongoro Mkoa wa Arusha na mauaji ya askari wa uhifadhi katika Kijiji cha Utimile Wilaya ya Sikonge Mkoa wa Tabora.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Afisa Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo Constantine Akitanda (pichani) tukio la Ndutu ni mauaji ya makusudi kwa sumu dhidi ya simba wakati tukio la Tabora lilitokea usiku wa kuamkia tarehe 18 Septemba 2026 baada ya askari kukamata mifugo iliyokuwa ikichungwa kinyume cha sheria ndani ya Pori la Akiba la Iswagala.
Taasisi imesema waliofariki katika tukio la Tabora ni watumishi wa uhifadhi waliokuwa wakitekeleza majukumu yao ya kulinda rasilimali za taifa na kwamba taarifa za awali zinaeleza watuhumiwa walitumia silaha za jadi kuwaua.
TCHI imesema matukio hayo ni pigo kubwa kwa urithi wa taifa na tishio kwa uhifadhi na uchumi wa utalii nchini. Taasisi imeonya kuwa pengo kati ya maneno ya kisiasa kuhusu kuishi pamoja na wanyamapori na uhalisia wa ardhini linazidi kupanuka na kwamba kuishi pamoja hakuwezi kuwa kauli mbiu ya mikutano bali ni lazima liwe uhalisia unaosimamiwa kikamilifu.
Aidha taasisi imetoa wito kwa Serikali kuharakisha uchunguzi wa kitaalamu na kuhakikisha haki inatendeka kwa haraka bila upendeleo na kwa vyombo vya ulinzi na usalama kuwasaka na kuwakamata wahusika wote wa mauaji ya watumishi hao.
Pia imetaka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na mashirika ya uhifadhi kuimarisha ulinzi wa askari wa mstari wa mbele na kudhibiti matumizi haramu ya viuatilifu vya kilimo.
TCHI imesisitiza kuwa wanasiasa wanapaswa kuacha tabia ya kuhurumia au kuwalinda watuhumiwa wa uhalifu wa wanyamapori mara wanapokamatwa na kwamba uhalifu huo na mauaji ya askari wa uhifadhi havipaswi kufanywa siasa.






0 Comments