Na Matukio DaimaMedia
Wadau wa demokrasia nchini wametaka Serikali, vyama vya siasa, viongozi wa dini na makundi mengine kukaa pamoja na kuzungumza kuhusu changamoto za kisiasa, mauaji na watu waliopotea ili kupata suluhisho na kujenga amani nchini.
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Demokrasia, mtaalamu mwandamizi nchini na Mwenyekiti mstaafu wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bahame Tom Nyanduga, alisema Tanzania inapaswa kwanza kutafuta ukweli kuhusu yaliyotokea katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Amesema kuwa, watu wengi walipoteza maisha siku hiyo na siku zilizofuata, huku wengine wakipotea na hadi sasa hawajulikani walipo.
Nyanduga amesema suala hilo haliwezi kupuuzwa, kwani limeacha maumivu kwa familia na jamii, hivyo Serikali inapaswa kuhakikisha ukweli unajulikana na waliohusika wanabainishwa.
Ameongeza kuwa, pia kuna haja ya kuangalia changamoto zilizopo katika sheria na mfumo wa uchaguzi ili kuhakikisha uchaguzi ujao unakuwa huru na wa haki.
Kwa mujibu wa Nyanduga, mazungumzo yanapaswa kuwahusisha Serikali, vyama na makundi mbalimbali, waathirika pamoja na ndugu wa waliopoteza maisha ili kujenga msingi wa maridhiano.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga, amesema demokrasia si uchaguzi pekee.
Amesema demokrasia pia ni pamoja na uhuru wa kutoa maoni, kupata taarifa, uhuru wa vyombo vya habari, kuheshimu haki za binadamu na kuhakikisha sheria inatumika kwa usawa.
Henga amesema hali ya demokrasia nchini ina changamoto, akitaja watu waliopoteza ndugu, wengine kutokujua walipo ndugu zao na wengine kuwa katika mazingira ya kifungo.
Aidha, ameema pia kuna malalamiko kuhusu uhuru wa vyombo vya habari na watu kukamatwa kutokana na maoni wanayotoa kwenye mitandao ya kijamii.
Henga ameongeza ni muhimu mazungumzo yaendelee ili wadau wajadiliane kuhusu hali hiyo na namna ya kuisogeza nchi mbele.
Alipendekeza pia mjadala kuhusu Katiba mpya uendelee, akisema Katiba mpya inaweza kusaidia kushughulikia sehemu kubwa ya changamoto zilizopo.
Naye Katibu Shura ya Maimamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda, amesema Tanzania inapitia mazingira magumu kisiasa ambayo yameathiri pia usalama na umoja wa wananchi.
Ponda amesema mjadala kuhusu Katiba umeibua mitazamo tofauti. Wapo wanaotaka Katiba mpya, wanaotaka marekebisho ya Katiba iliyopo, wanaotaka Katiba ya muda na wananchi wenye mitazamo tofauti kuhusu suala hilo.
Ameongeza tofauti hizo hazipaswi kuwagawa Watanzania, bali ziwe sababu ya watu kukutana, kusikilizana na kutafuta njia ya pamoja.
Ponda amesema mazungumzo ya kitaifa ni muhimu kwa sababu yanaweza kusaidia kufikia mwafaka na maridhiano.
Ameongeza kuwa, katika maridhiano, ni muhimu pia kuangalia maumivu ya familia za watu waliouawa na wale waliopotea.
Ponda amesema viongozi wa dini, vyama vya siasa na makundi mengine wanapaswa kuendelea kukutana na kuzungumza kuhusu matatizo hayo ili kufikia mwafaka na kujenga umoja wa kitaifa.










0 Comments