Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imepokea msaada wa mashine mbili za darubini zenye thamani ya TZS. 70 Mil kupitia mradi wa utafiti kwa wagonjwa wa saratani, zitakazoongeza uwezo wa wataalamu kufanya uchunguzi sahihi na wa mapema, kuwezesha utambuzi wa haraka wa ugonjwa na kuwasaidia wagonjwa kupata matibabu stahiki kwa wakati.
Mradi huo umefadhiliwa na University of California, San Francisco (UCSF) kupitia Hellman Fund, kwa kushirikiana na Global Cancer Program na Institute for Global Health Sciences, kwa lengo la kuimarisha tafiti za saratani na kuongeza uwezo wa MNH katika kutoa huduma za uchunguzi na matibabu kwa wagonjwa.
Akizungumza wakati wa kupokea mashine hizo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi, Dkt. Mbonea Yonazi, amesema msaada huo utaongeza uwezo wa hospitali katika kufanya uchunguzi wa saratani kwa usahihi na kwa wakati.
Dkt. Mbonea amesema mradi huo, pamoja na kusaidia kuboresha matibabu ya saratani, unalenga pia kuimarisha uchunguzi na utafiti unaohusiana na saratani, jambo litakalosaidia kuongeza uelewa wa ugonjwa huo na kuboresha huduma kwa wagonjwa. MNH itaendelea kushirikiana na taasisi za utafiti na wadau mbalimbali katika kuimarisha teknolojia, utaalamu na huduma za kibingwa na ubingwa bobezi.









0 Comments