Header Ads Widget

EACOP YALIPA FIDIA SH. 35.6 BILIONI

 

Na Matukiodaima Media-SINGIDA.

‎Zaidi ya Sh. Bilioni 35.6 zimetumika kulipa fidia kwa wananchi 10,144 kati ya 10,223 waliostahili kulipwa, ili kupisha utekelezaji wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), sawa na asilimia 99.5 ya walengwa, tangu kuanza kwa mradi huo mwaka 2016.

Afisa Uhusiano wa TPDC, Francis Mpokela, amesema hayo wakati wa mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari wa Mkoa wa Singida kuhusu miradi ya mafuta na gesi,.na amesema kuwa wananchi 294 wamejengewa nyumba, 340 wamepatiwa mafunzo ya ujasiriamali na mikopo, huku wananchi 9,347 wakipata ajira kutokana na utekelezaji wa mradi huo.

‎Mpokela amesema wananchi 45 bado wanaendelea na hatua za malipo baada ya kukamilisha taratibu zinazohitajika. 

Kwa upande mwingine, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Boaz Kajigili, amesema mafunzo hayo yatawasaidia waandishi kuelewa miradi ya mafuta na gesi na mchango wake katika maendeleo ya Taifa na mkoa.

‎Kajigili amesema TPDC ilianzishwa kupitia Tamko la Rais Na. 140 la Mei 30, 1969 na kuanza shughuli rasmi mwaka 1973. 

Chini ya Sheria ya Petroli Na. 21 ya mwaka 2015, TPDC inatambuliwa kama Kampuni ya Kitaifa ya Mafuta na ina majukumu yanayohusu utafiti, uzalishaji, uchakataji, usafirishaji, usambazaji, uwekezaji, ajira na biashara katika sekta ya mafuta na gesi.


‎Mratibu wa Mradi wa EACOP na TPDC, Aldo Makendi, amesema hadi sasa visima 96 vimechimbwa nchini, huku maeneo ya mabonde ya utafutaji yakifikia takribani kilomita za mraba 534,000. 

Kwa Singida, amesema utafiti wa mafuta wa Eyasi-Wembere unaoendelea katika maeneo ya Mkalama na Iramba unahusisha ukusanyaji na uchakataji wa data za mitetemo pamoja na maandalizi ya kisima cha utafutaji.

‎Mhandisi Mwandamizi wa TPDC, Hassan Temba, amesema kilomita 760 za data za mitetemo ya 2D zimekusanywa na maandalizi ya kilomita 321 za ziada yanaendelea. 

Amesema utafiti huo unaweza kufungua fursa za ajira, huduma, usafirishaji, biashara na uwekezaji iwapo mafuta yatathibitishwa kuwepo kwa kiwango cha kuzalishwa kibiashara.

 Amebainisha kuwa EACOP inapita katika mikoa nane ya Tanzania kwa urefu wa kilomita 1,147, huku TPDC ikiwa na asilimia 15 ya hisa katika EACOP Ltd kwa niaba ya Serikali.

‎MWISHO

MATUKIO DAIMA MEDIA IMETEULIWA KUWANIA TUZO ZA SKA2026 TUNAOMBA KURA YAKO WAWEZA KUPIGA KURA KIRAHISI KULIKO KUPITIA LINK HII CHINI ⬇️⬇️⬇️

BONYEZA HAPA KUPIGA KURA ZOTE NNE

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI