Wakazi wa Tigray, nchini Ethiopia, wameanza kununua chakula na bidhaa muhimu kwa wingi kutokana na hofu kwamba mapigano yaliyoanza Jumatano yanaweza kuongezeka.
Katika mji mkuu wa Tigray, Mekelle, wakazi wameripotiwa kununua kwa wingi chakula na mahitaji muhimu ya kila siku, huku wakihofia kurejea kwa hali kama ile iliyoshuhudiwa wakati wa vita vilivyopita, Reuters imeripoti.
Jana, vikosi vya Tigray viliteka viwanja vitatu vya ndege na kusema vimewaamuru wanajeshi wao “kuchukua hatua” kukabiliana na kile walichodai kuwa ni “mashambulizi yanayofanywa dhidi yao.”
Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya wamezitaka pande zinazopigana kusitisha mapigano na kurejea kwenye Makubaliano ya Pretoria, yaliyosaidia kumaliza vita vya miaka miwili vya Tigray.
Getachew Radda, mshauri wa Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, kuhusu masuala ya Afrika Mashariki na aliyewahi kuongoza Serikali ya Mpito ya Tigray, alisema kupitia mtandao wa X kwamba vikosi vya TPLF “vimeanzisha vita.”
“Tunanunua kile tunachoona tunahitaji,” wakazi waliiambia Reuters kwa njia ya simu.
Wakazi hao, ambao waliomba majina yao yasitajwe, walisema hali ya usalama imekuwa ngumu na imekuwa “vigumu kununua au kupata mahitaji ya msingi.”
Mmoja wao alisema: “Iwapo hali itakuwa kama vita vya awali, huenda mji ukazingirwa.”
Wakazi pia wamesema vikosi vya usalama vimeanza kupelekwa mitaani katika mji wa Mekelle, huku sauti za ndege zisizo na rubani zikisikika na hofu ikiongezeka kwamba upatikanaji wa chakula unaweza kuvurugika.
Mkazi mwingine wa Adigrat alisema maduka yameanza kuwa matupu baada ya wananchi kununua chakula kwa wingi kwa wakati mmoja.
Wakazi hao wawili pia walisema walishuhudia vijana wakilazimishwa kujiunga na jeshi, hali iliyozua hofu miongoni mwa wananchi.
“Nilimwona kijana mwenye umri wa miaka 18, ambaye alipoteza baba yake katika vita vilivyopita, akichukuliwa kwa lazima,” alisema mkazi mmoja wa Adigrat.
Vita vya awali vilivyodumu kwa miaka miwili vilisababisha uhaba mkubwa wa chakula, fedha na dawa.
Mapigano katika eneo la Tigray yalianza tena Februari 13, baada ya vita vya miaka miwili kumalizika kupitia Makubaliano ya Pretoria.
Kwa nini mahasimu wa zamani Ethiopia sasa wameungana?






0 Comments