Header Ads Widget

VIJANA 48 WAHITIMU MAFUNZO YA KIDIGITALI DIT, WAFUNGULIWA MILANGO YA AJIRA NA UJASIRIAMALI

 Na Mwandishi Wetu.

Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) imehitimisha mafunzo ya mradi wa majaribio wa kuwawezesha vijana kutumia teknolojia ya kidigitali katika kujitangaza, kujiajiri na kuongeza fursa za ajira, huku vijana 48  ( kwa upande wa DIT ) waliohitimu mafunzo hayo wakikabidhiwa vyeti vya utambuzi wa ushiriki wao.




Hafla fupi ya kufunga mafunzo hayo imefanyika leo, Septemba 25, 2026, ikiwa ni hatua muhimu katika juhudi za Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia za kuwawezesha vijana nchini kutumia ujuzi wa kidigitali kujiletea maendeleo na kuchangamkia fursa zinazotokana na ukuaji wa uchumi wa kidigitali.

Mafunzo hayo ni sehemu ya mradi wa majaribio unaolenga kuimarisha uwezo wa vijana wa elimu ya juu katika matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA), hususan katika kutangaza ujuzi, ubunifu, bidhaa na huduma zao kupitia majukwaa ya kidigitali.

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Kaimu Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Prof. Ezekiel Amri, amewapongeza vijana hao kwa kuhitimu mafunzo hayo na kuwataka kutumia maarifa na ujuzi walioupata kwa malengo chanya yatakayowasaidia kujiajiri au kuongeza uwezekano wa kuajiriwa.

Prof. Amri amesisitiza kuwa teknolojia ya kidigitali inapaswa kuwa nyenzo ya maendeleo kwa vijana, hivyo kuwataka kuitumia kwa ubunifu na tija katika shughuli zao za kiuchumi na kijamii, badala ya kuitumia kwa mambo yasiyokuwa na manufaa.

Aidha, amewahimiza wahitimu hao kuendeleza mshikamano na ushirikiano walioanzisha wakati wa mafunzo, akieleza kuwa kuendelea kubadilishana maarifa, uzoefu na fursa kutawasaidia kukua zaidi katika shughuli zao za kitaaluma na kibiashara.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kituo cha Umahiri wa TEHAMA cha DIT, kinachofahamika kama India–Tanzania Centre of Excellence in ICT, Bw. Finian Mwalongo, amesema vijana hao wamepata ujuzi muhimu wa kidigitali utakaowasaidia kujitangaza kitaalamu, kukuza biashara zao na kuongeza fursa za kupata ajira.

Amesema mafunzo hayo yamewajengea vijana uwezo wa kutumia majukwaa ya kidigitali kuwasilisha ujuzi na huduma zao kwa namna itakayorahisisha kufikiwa na wateja, waajiri na wadau wengine wanaohitaji huduma zao.

Bw. Mwalongo amebainisha kuwa DIT itaendelea kutoa mafunzo hayo kwa vijana wengine kupitia awamu ya pili, ikiwalenga zaidi wale walioomba kushiriki katika awamu ya kwanza lakini hawakupata nafasi kutokana na idadi ya nafasi zilizokuwepo.

“Mafunzo haya kwa hapa DIT ni ya awamu ya kwanza. Tutakuwa na mafunzo ya awamu ya pili kwa kundi la vijana, hasa wale walioomba lakini nafasi hazikutosha. Wiki ijayo tutaanza mafunzo mengine kwa vijana wengine.

“Lakini pia, kama DIT, tutaendelea kuwa na hawa vijana, kuwaongoza na kuhakikisha mafunzo haya waliyoyapata na ambayo wataendelea kuyapata yanawanufaisha kama ambavyo Serikali yetu ililenga,” amesema Bw. Mwalongo.

Amesema DIT itaendelea kushirikiana na vijana hao kwa kuwapa mwongozo na kuwawezesha kutumia maarifa waliyojifunza katika mazingira halisi ya kazi na biashara, ili mafunzo hayo yawe na matokeo yanayoonekana katika maisha yao.

Kauli hiyo inaonesha dhamira ya DIT ya kutekeleza jukumu lake la kuendeleza ujuzi wa kiteknolojia kwa vitendo, sambamba na kuwaunganisha vijana na fursa zinazoweza kuchochea ubunifu, ujasiriamali na ajira.

Naye Nayfath Mohammed Abdallah, mmoja wa vijana walionufaika na mafunzo hayo, ameipongeza Serikali kwa kuanzisha programu hiyo, akisema imewapa vijana fursa ya kujifunza namna ya kutumia teknolojia ya kidigitali kutangaza na kukuza shughuli zao.

Nayfath amesema licha ya muda wa mafunzo kuwa siku tano pekee, washiriki wamejifunza mambo mengi yenye manufaa, huku baadhi yao wakianza kuona matokeo ya moja kwa moja kupitia upatikanaji wa wateja wa biashara zao kwenye majukwaa ya mtandaoni.

Ameomba mafunzo hayo yaendelee kutolewa kwa vijana wengine, huku akishauri muda wa mafunzo uongezwe ili washiriki wapate nafasi ya kujifunza kwa kina zaidi na kumudu stadi nyingi zaidi za kidigitali.

Amesema mafunzo hayo yamekuwa chachu ya kuwapa uelewa mpana kuhusu namna ya kutumia teknolojia kujitangaza, kufikia wateja wengi zaidi na kupanua wigo wa shughuli zao za kiuchumi.























































Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI